January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

SMZ yafunga kituo cha radio Z’bar

Spread the love

KADHIA ya ufutwaji uchaguzi wa Zanzibar ikiwa haijapatiwa ufumbuzi, kumekuwa na hatua za ukandamizaji wa uhuru wa habari hapa Zanzibar na tayari madhara yametokea. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilichukua hatua katili tarehe 26 Oktoba 2015, ilipoamuru kufungwa kwa kituo kipya cha redio cha Swahiba FM kwa maelezo kuwa kimevunja sheria.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Kassim Suleiman ameiambia MwanaHALISI Online, kwamba kituo hicho kilifungwa kwa uonevu kwa sababu “hata utaratibu wa kisheria haukufuatwa.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Utangazaji ya Zanzibar, amesema hatua kama hiyo huchukuliwa baada ya mmiliki wa kituo chenyewe kufahamishwa na kuwa amepewa nafasi rasmi ya kujitetea baada ya kujulishwa kosa linalodaiwa kuwa limefanywa na kituo.

Kassim ambaye aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) kabla ya kubadilishwa na kuwa Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), alisema amelalamika rasmi kwa barua kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Kosa lililotajwa kuwa kituo hicho kimefanya ni kutangaza tamko la Maalim Seif Shariff Hamad la Oktoba 26 la kwamba alikuwa anaonesha kuwa na kura nyingi na kutaka Tume ya Uchaguzi itangaze matokeo bila ya kuchelewa.

Taarifa za ndani ya Tume ya Utangazaji zinasema uamuzi huo wa kufunga kituo cha Swahiba FM, kinachoendeshwa na kampuni inayomilikiwa na Chama cha Wananchi (CUF), umechukuliwa bila ya Bodi ya Tume kujua.

Kisheria uamuzi wowote kama huo utachukuliwa baada ya Bodi kujadili tuhuma na kutoa uamuzi wake. Mjumbe mmoja wa Bodi hiyo ameithibitishia MwanaHALISI Online, kuwa hawakukaa kujadili suala hilo.

Juzi askari wa Jeshi la Polisi walivamia maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar na kukamata wauza magazeti, na kukamata wafanyakazi wa duka la vitabu na machapisho la BMC kwa kuwa lilikuwa likitoa nakala za gazeti la MwanaHALISI la Jumatatu baada ya gazeti hilo kutoonekana mitaani muda mfupi lipobainika.

error: Content is protected !!