January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sitti Mtemvu atema taji Miss Tanzania 2014

Aliyekuwa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu alipotawazwa kutwaa taji hilo akiwa na washindi wa pili na watatu

Spread the love

TUHUMA za kufanya udanganyifu, ikiwemo kughushi umri, ili kushiriki shindano la kutafuta mrembo wa Taifa – Miss Tanzania 2014 – zimemgharimu Sitti Mtemvu ambaye sasa amelivua taji.

MwanaHALISI Online limeiona barua aliyoiandika Sitti mwenyewe akitangaza kuwa amejivua taji hilo alilovikwa Oktoba 10, kwa kile alichoita “kuzuka kwa shutuma za uongozi dhidi yangu.”

“Mimi Sitti Abas Mtemvu, kwa hiyari yangu mwenyewe tena bila ya kushawishiwa na mtu na kwa kulinda heshima yangu pamoja na familia yangu, natamka rasmi kuvua taji la urembo la Miss Tanzania 2014,” imesema barua.

Sitti ni mtoto wa Mbunge wa Temeke, jijini Dar es Salaam, Abass Zuberi Mtemvu, ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alifunga safari kutoka nchini Marekani alikokuwa anasoma, kuja nchini kushiriki mashindano ya urembo.

Alianza mbali katika mpango wake wa kujenga jina kupitia ulimbwende. Alianzia na kushiriki shindano la kitongoji cha Chang’ombe, na kushinda taji. Akaingia shindano la Mkoa wa Temeke (Miss Temeke) ambako pia alitangazwa mshindi na kuvikwa taji.

Kwa kutwaa taji la Mkoa, Sitti alipata tiketi ya kushiriki shindano la ngazi ya taifa, ambalo huandaliwa na asasi ya Lino International Agency inayomilikiwa na Hashim Lundenga, muanzilishi wa mashindano ya urembo nchini yaliporuhusiwa tena mwaka 1994, baada ya kupigwa marufuku mwaka 1968 na Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere.

Mara baada ya shindano la taifa, zikaibuka tuhuma dhidi ya Sitti, kwamba alidanganya umri akitaja ana umri wa miaka 24, wakati ilisemekana amefikia miaka 25. Umri wa mwisho kuruhusiwa kushiriki urembo nchini ni miaka 24.

Lakini pia Sitti, akasemekana tayari ana mtoto wa kuzaa, jambo linalomnyima sifa ya kushiriki urembo kwa kuwa mshindani hatakiwi kuwa na mtoto.

Pamoja na tuhuma hizo kutolewa huku vikioneshwa vielelezo vya kuzaliwa kwake, pasipoti yake na mtoto anayesemekana ni wake, Sitti alikanusha yote.

Mbele ya waandishi wa habari wiki mbili zilizopita, akiandamana na Lundenga, Sitti alipojitokeza baada ya tuhuma kuenea, alisema anasakamwa isivyo halali kwa mambo ya kusingizia.

Hapo akatoa mwanya kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini – Registration, Insolvency and Trusteeship Agency (RITA) – kujitokeza na kuahidi kuwa itachunguza uhalali wa cheti chake cha kuzaliwa ili kujiridhisha na umri halali wa Sitti.

Hata Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ndilo husimamia maendeleo ya sanaa nchini, likiwa chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, lilisema ikithibitika amedanganya, lazima atavuliwa taji.

Tuhuma dhidi ya Sitti zilipoibuliwa, muandishi mmoja wa mtandao wa kijamii alipenyeza hati ya kusafiria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyotolewa 17 Februari, 2007 na mwisho wa uhalali wake kuwa 14 Februari, 2017.

Hati hiyo inaonesha Sitti alizaliwa Mei 31, 1989 na hivyo kuwa ni msichana wa umri wa miaka 25 kwa sasa.

Pia ilipenyezwa mtandaoni leseni yake ya kimataifa ya udereva iliyotolewa na Serikali ya jimbo la Texas, nchini Marekani tarehe 26 Machi, 2013. Uhalali wa leseni hiyo ambayo pia imebainisha siku ya kuzaliwa kwake ni 31 Mei 1989, unakoma tarehe 30 Oktoba, 2015.

Haikufahamika kama uchunguzi wa tuhuma umekamilika na nini kilichothibitishwa, lakini Jumamosi hii, Lundenga aliita waandishi wa habari na kutangaza kuwa Sitti amejivua taji.

Akizungumza katika mkutano huo, Lundenga, ambaye naye sasa anavutana na muanzilishi mwenzake wa mashindano ya urembo, Prashant Patel, kwanza alisema amekuja tu na barua bila ya Sitti mwenyewe kufika mkutanoni.

Alisema barua hiyo iliandikwa na Sitti tarehe 5 Novemba, 2014 akiituma kwake Lundega. Aliipokea siku ya pili yake.

“Baada ya kutokea malalamiko kuhusu umri wa Sitti, iliundwa kamati kuchunguza ukweli wa jambo hili. Waandaaji tumepokea maelekezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, na barua ya Sitti mwenyewe ninayo hapa nitawasomea,” alisema Lundenga bila ya kueleza sababu za msingi za Sitti kutokuwepo.

Katika barua yake hiyo, Sitti amelalamika tu kuwa amezushiwa tuhuma ambazo zimeandikwa kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii, lakini hakutaja hata tuhuma moja.

Shindano la Miss Tanzania 2014 lilifanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambako mara baada ya kutangazwa ndiye mshindi, Sitti alijinasibu ana umri wa miaka 18 na kielimu, ana shahada mbili.

Kwa kuwa wapo wanaojua historia yake kwa kuwa alizaliwa na kukulia jijini Dar es Salaam, maelezo yake hayo yalichochea kuhojiwa uhalali wake.

Tuhuma zilipovuma kwamba amedanganya umri, Mwanahalisifoum.com nayo ilitoa undani wa tuhuma hizo, na wimbi hilo likamsukuma Sitti kuomba kuandamana na Lundenga kutoka hadharani kujieleza.

Hakutoa maelezo yaliyoridhisha waandishi wa habari, lakini bado baba yake, Mtemvu anayemiliki asasi inayosaidia vijana kupata ajira nchi za nje, pamoja na mkewe, walimtetea Sitti. Mara hii baadhi ya vyombo vya habari vilitumika kuipa familia yake nafasi ya kueleza ukweli wa upande wao.

Hatimaye, Sitti ameamua kutenda kilichotarajiwa. Amekubali yaishe akiamini atapata utulivu upya na kuendelea na shughuli zake za kimaisha.

Baada ya uamuzi wake, Lundenga alimtangaza Lilian Kamazima, aliyekuwa mrembo wa pili bora baada ya Sitti, kuwa ndiye Mrembo wa Taifa 2014 atakayewakilisha nchi kwenye shindano la dunia mapema mwakani.

Wakati wa shindano, nafasi kubwa ya kutwaa taji ilionekana kumuangukia mrembo mwenye asili ya Kihindi, Jihan Dimachk aliyetangazwa mshindi wa tatu.

Tukio la mrembo wa taifa kujivua taji ndio la kwanza kutokea nchini. Nalo linathibitisha manung’uniko ya muda mrefu kwamba siku hizi limekuwa ni shindano linalogubikwa na tuhuma za upendeleo.

error: Content is protected !!