July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sitta, Werema maadui wapya wa Katiba Mpya

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Jaji Fredrick Werema akitoa mchango wake kwenye Bunge Maalum la Katiba.

Spread the love

JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limesema Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel John Sitta na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema ni “Maadui wapya wa Katiba Mpya Tanzania”

Deus Kimbamba, mwenyekiti wa JUKATA amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kwamba Sitta ambaye ni Waziri wa Masuala ya Africa Mashariki na Mbunge wa Urambo Mashariki amekuwa kinara wa kushambulia vyombo vya habari na watu binafsi kana kwamba Katiba Mpya ni mradi wake binafsi huku akijua kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu wa uandishi wa katiba mpya.

Pia, amekuwa kinara wa upotoshaji katika siku za karibuni akitamka mambo kadhaa huku akijua kuwa si ya kweli.

“JUKATA tunaona hatari kubwa ya upotoshaji wa kimakusudi kwa Katiba. Tumekuwa na utamaduni wa kutoa hati chafu kwa wavurugaji wa mchakato wa katiba. Kwa jinsi hiyo hiyo, leo tunawatangazia rasmi maadui wawili wa Katiba Mpya ambao ni; Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema”

Akitolea mfano wa matamshi hayo Kimbamba amesema “Tamko lake kuwa hadhi ya Bunge Maalum la Katiba iko juu kidogo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni upotoshaji wa makusudi kwa kuwa vyombo hivi vina hadhi sawa kwa mizani yoyote ile”

Kimbamba amesema Sitta amesikika akisema kuwa pamoja na makubaliano ya kuahirishwa kwa mchakato wa Katiba hadi baada ya uchaguzi mkuu, upigiaji kura rasimu ya Katiba kifungu kwa kifungu uko palepale.

Licha ya uwezekano wa theluthi mbili kutopatikana na kwamba utaratibu utafanywa ili hata wajumbe walio nje ya nchi wakihudhuria ibada ya hija, wagonjwa walio vitandani India na kwingineko pamoja na wawaziri walio safarini ughaibuni nao wataweza kusomewa Rasimu ‘mpya’ kifungu kwa kifungu kabla ya kupiga kura huko huko waliko.

“Ni wazi kuwa Mheshimiwa Sitta anafanya haya huku akijua kuwa anapotosha umma kwa kuwa mipango ya miaka mingi hata kuwezesha watanzania walioko nje ya nchi kupiga kura haijawahi kufanikiwa,” amesema Kibamba.

Aidha, tamko lake linaleta hisia kuwa anataka kutumia upenyo wa walio nje ya nchi kuchakachukua idadi ya kura za ndiyo kwa rasimu ya Katiba. Sitta ameamua kuendelea na Bunge Maalum la Katiba huku akijua kuwa kutokuwepo kwa idadi ya wajumbe kiasi hicho ni doa kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Kimbamba amesema Sitta amekuwa kinara wa kuwaaminisha watanzania kuwa Katiba Mpya itapatikana bila tatizo pamoja na kutokuwepo kwa ushiriki wa UKAWA, Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar Abubakary Khamis Bakary na hata Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman.

“Haya yanafanywa huku Sitta, ambaye ni mtumishi mwandamizi katika serikali ya Tanzania kwa miaka takribani 50 na bungeni kwa miaka 40 sasa akiwa anafahamu fika kuwa Katiba ni suala ya maafikiano, makubaliano na maridhiano kati ya nchi mbili zilizoungana mwaka 1964 yaani Tanganyika na Zanzibar na kususa kwa vigogo hawa muhimu wa SMZ ni sawa na kususa kwa Zanzibar na kunaondoa uhalali wa Katiba itakayopendekezwa.

Kimbamba amesema Jaji Frederick Werema , akiwa nguli wa tasnia ya Sheria na mshauri mkuu wa sheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa bingwa wa kutoa tafsiri tata ndani na nje ya Bunge kuhusu mchakato wa Katiba mpya.

“Kwanza, aliwahi kushauri kuwa tafsiri ya siku 70 za Bunge Maalum ni pamoja na siku za mapumziko na sikukuu na kufanya Bunge kufanya kazi hadi Jumamosi katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo,” amesema Kimbamba.

Kimbamba amesema kuwa Werema aliendelea kutoa tafsiri tofauti na kupelekea Bunge maalum kubadili utaratibu na kuanza kupumzika siku za Jumamosi, Jumapili na sikukuu katika awamu ya pili na hivyo kukiuka amri ya Rais kupitia tangazo la serikali (GN).

Ni katika hali hiyo kulitokea mkanganyiko wa endapo Bunge liishie tarehe Oktoba 4 au 31 Oktoba huku yeye akikubaliana na yoyote katika tarehe hizo.

“Pili, Werema amekuwa mshauri mbaya wa Bunge Maalum la Katiba akimwaminisha Mwenyekiti wake, wabunge waliomo ndani na watanzania kuwa mchakato wa Katiba utakamilika hata bila ya wajumbe wote hao walio nje na mahudhurio duni,” amesema Kimbamba.

Aidha, amesema Werema amekuwa kinara wa kushauri kuwa muundo wa serikali tatu ulio katika rasimu unaweza kubadilika kiuandishi na kuwa rasimu ya serikali mbili bila shida jambo ambalo linapingwa na wanasheria na wasomi wenzake wengi akiwemo Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Kimbamba amesema ni msigano huu ndio umeufikisha mchakato wa Katiba Mpya katika mgogoro mkubwa zaidi ukiacha ule uliotokana na UKAWA kutoka nje. Taifa litakumbuka kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar amemwandikia Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kujitoa katika kamati ya uandishi wa Katiba inayopendekezwa kwa kile anachoamini kuwa katiba mpya haiandikiki kwa mazingira ya ‘uchakachuaji’ na kwamba maslahi ya Zanzibar ‘yanakanyagwa’ kwa uchakachuaji huo.

“Kutokana na makosa hayo ya upotoshaji, JUKATA inawatangaza rasmi Samuel John Sitta, Jaji Frederick Werema kuwa Maadui wapya wa Katiba Mpya Tanzania. Kwa tangazo hili, JUKATA tunapendekeza kuwa watu hao wasifikiriwe kwa nafasi yoyote ya kuchaguliwa zikiwemo za Udiwani na Ubunge au kuteuliwa katika miaka kumi ijayo ili kutoa muda kwao kujitafakari kwanza” amesema Kimbamba.

error: Content is protected !!