January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sitta apangua tuhuma za Zitto

Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta (kulia) akiwa na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (katikati) na Mbinge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakiwa nje ya jengo la Bunge

Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta (kulia) akiwa na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (katikati) na Mbinge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakiwa nje ya jengo la Bunge

Spread the love

TUHUMA za ufisadi zilizotolewa na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe dhidi ya Serikali katika mradi wake mpya wa Mwambani Port and Railway Corridor Company (MWAPORC) Tanga, zimepanguliwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Jumapili iliyopita, Zitto akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Iringa, alisema kuna ufisadi mkubwa zaidi ya ule wa wizi wa fedha za Escrow katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) ambao unagharimu zaidi ya Sh.50 trilioni, ukifanywa na Mwenyekiti wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira.

Katika tuhuma hizo nzito, Zitto alisema serikali imetoa mradi kwa Rugemalira  kifisadi bila kuzingatia sheria ya kutangaza zabuni. Kwamba anashangazwa na serikali kuwapa kazi ya ujenzi ya bandari ya MWAPORC watu ambao walikuwa wanatuhumiwa katika kashfa ya akaunti Tegeta Escrow pasipo kufuata utaratibu.

“ACT – Wazalendo tunamtaka Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta afanye uchunguzi kuhusu mradi huo wa MWAPORC na achukue hatua  kwa kuwa huu ni ufisadi mkubwa kushinda ule wa Escrow,” alisema Zitto. 

Sitta katika mkutano wake na waandishi wa habari leo, ametumia dakika chache kujibu tuhuma za Zitto, akisema hakuna ufisadi wowote unaofanywa na serikali, bali watu mbalimbali wa sekta binafsi wanabuni miradi na kuja kuiombea vibali serikalini.

Amesema, “Rugemalira na watu wengine wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) wamekuwa wakijaribu kupata wabia ili kuendeleza mradi wao wakiwa na lengo nzuri kabisa kwamba tupate biashara inayotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Serikali haihusiki na senti yoyote ila tunasubiri mapendekezo yao yoyote kwa hatua za awali. Niseme tu haitakuwa rahisi kukubali mradi ambao unakwenda sambamba  na mradi wa reli ya kati, kwa sababu ni lazima tutazame faida itakayopatikana”.

Sitta ameongeza kuwa kama kuna kundi la Watanzania wanataka kushawishi basi waanzie kuangazia upande wa Congo ambapo ni takribani kilomita 2000 ambayo inaunganisha na reli ambayo ipo kwenye mradi.

“Kwa kuwa tuna mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha upana mpya yaani kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, Tabora, Mwanza, Isaka, Rusumo, Kariwa, Mpanda na Karemo. Huu ndio mpango uliopo wa serikali, na unatafutiwa fedha na tumefika pazuri.

“Yoyote anayetaka kuwekeza katika mradi huu aje, ila ni lazma kuwe na uwiano. Vinginevyo tunaweza kujenga reli mbili kwenda sehemu moja harafu tupate hasara, kwa hiyo hakuna mradi wowote ambao serikali imeingia ubia ukiacha mradi wetu,” amesema Sitta.

error: Content is protected !!