January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sitta aingia uwanjani na hoja 5

Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta, ametangaza nia ya kuutaka urais

Spread the love

WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ametangaza nia ya kuutaka urais wa Tanzania huku akiahidi kushughurikia kero za muungano, mchakato wa Katiba, uchumi, rushwa na kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, ametangaza nia hiyo jana katika mkutano uliofanyika viwanja vya Ikulu ya Chifu Fundikira, Kata ya Itetemia mkoani Tabora.   

Sitta amesema “nasimama mbele kwa unyenyekevu kuelezea kusudio la kukiomba CCM, kilichonilea tangu enzi za TANU kuniteua kuwa mgombea wake wa urais wa nchi yetu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.”  

“Ninazo sababu tano zilizonisukuma nifikirie kukiomba chama changu kiniteue kugombea nafasi hiyo. Binafsi naamini kuwa kipindi cha uongozi 2015 – 2020 ni kipindi chenye changamoto nzito za kitaifa ambazo zinahitaji aina ya uongozi wenye uimara, uadilifu, uzalendo na maarifa thabiti ili kuivusha nchi kwa usalama,” amesema Sitta.

Muungano 

Sitta amesema kumekuwepo na kauli na vitendo vinavyoashiria kuvunja muungano. Amevitaja baadhi ya vitendo hivyo kuwa baadhi ya wanasiasa kutoka Zanzibar kudai Zanzibar itanufaika zaidi ikiwa na uhuru kamili bila kuwa sehemu ya muungano.

Amesema kuwa baadhi ya wabara wanadai Zanzibar ni wakorofi, wasioridhika na chochote kinachofanywa na muungano. Hali ambayo itazua uhasama, udini na kuvunjika kwa amani.

“Ushiriki wangu katika serikali yetu tangu awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu unaniweka katika nafasi nzuri ya kuongoza mchakato utakaowezesha kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto za muungano,”ameeleza Sitta.

Mchakato wa Katiba

Kuhusu suala la Katiba mpya, amesema pamoja na kutopatikana kwa muafaka wakati wa Bunge Maalum la Katiba, lakini pande zinazosigana kuhusu Katiba zina wazalendo ambao wanaweza kukubaliana.

“Kwanza, hakuna mshindi wala mshidwa katika kufikia kukubalika kwa Katiba ya Taifa letu. Pili, Katiba yoyote ni waraka unaoenda unabadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika,” Sitta amefafanua.

Uchumi

Amesema ili kukuza uchumi wa nchi kwa kasi inayopunguza umasikini kwa haraka, atajenga uwezo mkubwa zaidi wa bajeti ya serikali kutosheleza ubora wa huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji.

Hivyo ni lazima jitihada za makudi za kubadili mfumo wa uendeshaji nchi uwe ni wa motisha kwa wazalishajimali. 

Rushwa

Kuhusu rushwa, Sitta ameeleza kuwa suala hilo limekidhiri katika mikataba mibovu ya huduma za mauzo, manunuzi hewa, manunuzi yaliyojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni na katika ajira na kusababisha hasara ya matrilioni ya fedha kwa taifa.

“Nitahakikisha kuwa miiko ya uongozi inarejeshwa na kutungiwa sheria ili kudhibiti ufisadi. Hatua ya pili ni kutunga sheria mpya zilizo kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa,” amefafanua Sitta.

Ili kufanikisha hilo amesema atahakikisha: Mali za viongozi zinatamkwa kwa uwazi, mali isiyolingana na kipato na kukosa maelezo ya kutosheleza inataifishwa, kesi za rushwa kuwa na utaratibu wenye uwazi, tume inayoshughulikia maadili ya viongozi inapewa nguvu na adhabu ya upokeaji na kutoa rushwa kuongezewa makali.

Kuimarisha uchumi wa  CCM

Mbali na ahadi hizo, Pia amesema atahakikisha vitega uchumi vya CCM vinakuwa na tija inayokiwezesha chama kuendesha shughuli zake kwa kujitegemea na kinga dhidi ya rushwa.

“Nikibahatika kuchaguliwa katika nafasi ya urais, nitatumia uzoefu wangu wa miaka tisa na nusu katika kukiongoza Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuziunganisha shughuli za uchumi za chama na wawekezaji makini ili kupunguza utegemezi wa ruzuku ya serikali ,” ameeleza Sitta.

Wasifu

Sitta alizaliwa 18 Disemba 1942. Amekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka 1987 hadi sasa. Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM mwaka 2005 – 2010. Spika wa Bunge la Tanzania 2005 – 2010. Uzoefu wake katika uongozi ni zaidi ya miaka 30.

error: Content is protected !!