SHIRIKA la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (Dawasco) linawashikilia mama ntilie sita kwa madai ya kutumia huduma ya maji kinyume cha utaratibu,anaandika Eunice Laurian.
Mama hao wanadaiwa kujiunganisha majisafi kienyeji katika Mtaa wa Kisutu, Ilala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la tukio Deogratius Ng’wandu, Ofisa Biashara wa Dawasco amesema kuwa, wamebaini wizi huo wakati wa operashani maalum inayoendelea kwa sasa kwenye maeneo yote Dar es Salaam.
“Tumewakuta mamantilie wakiwa wanatumia huduma ya maji ambayo imeunganishwa kinyume cha taratibu, maji hayo hayakuwa na mita wala akaunti namba,” amesema Ng’wandu.
Subira Ngeseyani, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kisutu amewaomba wananchi kutoa ushirikianao kwa kuwataja wezi wa maji katika mitaa yao kama ilivyoagiza na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Aziza Hassan ambaye ni mtuhumiwa amekiri kutumia huduma ya maji kinyume na taratibu za Dawasco kwa madai ya kutojua.
“Kweli tumekuwa tukitumia huduma ya maji kwenye eneo hili kwa kutojua kutokana na hali ngumu ya maisha lakini pia kuunganisha huduma hii ni gharama kubwa,” amesema Aziza.
More Stories
Huawei yaunga mkono malengo endelevu UN
Watuhumiwa 5 ujambazi wauawa Dar, bastola…
Takukuru yavimbia wakandarasi, ‘yarejesha’ mil 420 Tanesco