July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siri za Prof. Lipumba kujiuzulu zafichuka

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete (kulia), akifurahia jambo na Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

SIRI kuu ya kujiuzulu uenyekiti katika Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, imeanza kufichuka. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Taarifa kutoka serikalini, ofisi kuu ya CCM, Lumumba, Idara ya Usalama wa taifa (TISS) na kwa watu waliokaribu na Prof. Lipumba mwenyewe zinasema, kiongozi huyo amejiuzulu ili kulinda ajira ya mmoja wa maswahiba wake wakubwa serikalini.

“Prof. Lipumba amejiuzulu baada ya wakubwa ‘kufika bei’ ili kulinda kibarua cha mmoja wa vigogo kutoka idara nyeti serikalini, ambaye ni swahiba wake wa karibu,” ameeleza mmoja wa viongozi wajuu kutoka serikalini.

Haijafahamika kiasi gani cha fedha alicholipwa, ili kumshawishi kujiondoa katika wazifa wake, ingawa kuna taarifa kuwa zaidi ya Sh. 3.7 bilioni zimetumika kwa kazi hiyo.

Aidha, taarifa zinasema, Prof. Lipumba amelazimika kujiuzulu baada ya kuahidiwa madaraka makubwa katika serikali ijayo, ikiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitafanikiwa kushika madaraka ya dola.

Miongoni mwa vyeo ambavyo Prof. Lipumba ameambiwa atakabidhiwa, ni kufanywa kuwa waziri wa fedha katika serikali ya John Magufuli au kuwa mshauri mkuu wa uchumi wa serikali hiyo.

Kupatikana kwa taarifa kuwa Prof. Lipumba amelambishwa donge kubwa ili kusaliti mageuzi, zimekuja siku tatu baada ya mwanasiasa huyo aliyekuwa akiheshimika nchini kutangaza kujiuzulu kwa kile alichoita, “kusutwa na dhamira yake.”

Alisema, ameamua kujiuzulu wazifa wake wa unyekiti baada ya viongozi wenzake wanne kutoka jumuiko la vyama vinavyounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), kumkaribisha ndani ya umoja huo, mwanasiasa mashuhuri nchini, Edward Lowassa na kisha kumteuwa kuwa mgombea wake wa urais.

Vyama vinavyounda UKAWA, ni NCCR- Mageuzi, CUF, National Democrat League (NLD) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lowassa alijiunga na Chadema baada ya viongozi wakuu wa UKAWA, akiwamo Pro. Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Dk. Emanuel Makaidi, kukutana na kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu jambo hilo.

Vyanzo vya taarifa vinasema, Prof. Lipumba alikutana mara kadhaa na kwa faragha na Lowassa kwa lengo la kumshawishi kujiunga na umoja huo.

Miongoni mwa mikutano hiyo, ni pamoja ule uliofanyika Jumamosi ya tarehe 4 Aprili, majira ya saa 5 asubuhi, ofisini kwa Lowassa, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Prof. Lipumba alimhakikishia Lowassa kuwa UKAWA wako tayari kumpokea na kumkabidhi bendera yake katika kinyang’anyiro cha urais cha Oktoba. Alitumia mkutano huo kumkandia Dk. Willibrod Slaa kwa kudai kuwa siyo mtu mwenye sifa za kuwania nafasi hiyo, kwa madai kuwa ni mtu asiyeaminika.

Hata hivyo, Lowassa alimuonya mwanasiasa huyo kuwa makini na kauli zake kwa kuwa zitaweza kuwagawa. Alisema, anamfahamu vema Dk. Slaa na hana matatizo naye.

Habari zinasema, mara baada ya Prof. Lipumba kujiuzulu, aliondoka nchini kuelekea Rwanda kwa kazi maalum aliyopewa na CCM.

Akiongea na Azam Televisheni, Prof. Lipumba amekiri kuwa nchini Rwnada na kuongeza, “niko huku kufanya utafiti wa jinsi Rwanda ilivyofanikiwa kiuchumi,” jambo ambalo linathibitisha madai kuwa atakuwa mshauri wa uchumi au waziri wa fedha katika serikali ya CCM.

Mtoa taarifa anasema, Pro. Lipumba ameondoka nchini na walinzi maalum ambao amekabidhiwa kama sehemu ya makubaliano ya mradi wake na serikali.

Anasema, “…hii habari ya Lipumba imethibitisha kile nilichokisema siku za nyuma, Lipumba anatumika. Ni kibaraka… Tena hukutana naye nyumbani kwake.

“Nilipoona Prof. Lipumba yuko UKAWA nilipata mashaka makubwa, lakini nilikuwa na ahueni kwa sababu niliambiwa Maalim Seif Sharif Hamad, alishawatahadharisha wenzake wasimshirikishe Lipumba kwenye mambo nyeti ya UKAWA kwa sababu haaminiki.”

error: Content is protected !!