July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siri za kuvuruga uchaguzi zaanikwa

Spread the love

ZIKIWA zimebaki siku tatu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefichua mikakati iliyopangwa kuvuruga uchaguzi huo. Anaandika Charles William … (endelea).

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi amebainisha mipango ‘ovu’ inayoratibiwa ili kuvuruga uchaguzi mkuu huku mipango hii ikishirikisha baadhi ya makampuni ya simu za mkononi, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na wakurugenzi wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali.

Munisi ametaja baadhi ya mipango hiyo kama ifuatavyo, huku akitahadharisha watakaoshiriki mipango hiyo kuwa wataliingiza taifa katika machafuko bila sababu ya msingi.

Mpango wa kukata mawasiliano ya simu na data; upo mpango wa kuzuia mawasiliano ya simu za mkononi kwa kusitisha huduma ya kupiga na kupokea simu, kuzuia ujumbe mfupi wa maneno (sms), kuzuiwa kwa intaneti (data) na hivyo mawasiliano kuwa magumu, hasa wakati wa matokeo kubandikwa vituoni.

Mpango huu unatajwa kuwa na lengo la kukwamisha watu kuwasiliana na kupeana matokeo yatakayokuwa yakibandikwa vituoni ili kujumlisha na kupata matokeo ya jumla ya nafasi za udiwani, ubunge na urais. Utekelezaji wa mpango huu utashirikisha baadhi ya makampuni ya simu ambazo hakutaka kuzitaja.

“Tunaziomba kampuni za simu zenye mpango huo, kuacha mara moja kwani zitajiongeza katika orodha ya watuhumiwa watakaoenda ‘The Hague’ mara baada ya uchaguzi kumalizika,” alieleza Munisi bila kuyataja makampuni hayo kwa kuwa bado chama hicho kinakusanya vielelezo.

Mpango wa kukata umeme maeneo yenye nguvu kubwa ya upinzani; maeneo ambayo vyama vya upinzani vina nguvu kubwa umeme utakatwa baada ya giza kuingia ili kuhakikisha mchakato wa kuhesabu na kujumlisha matokeo unaingia dosari na hata vurugu kutokea ili katika taharuki hiyo wizi wa kura uweze kufanyika.

Baadhi ya wakurugenzi wa uchaguzi kutoruhusu mawakala wa akiba wa upinzani kuapishwa; wakati uapishaji wa mawakala ukiendelea katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi ya maeneo vyama vya upinzani vinazuiwa kuapisha mawakala wa akiba na wakurugenzi kutaka mawakala waape idadi sawa na idadi ya vituo vya kupigia kura.

Mkakati huu unalenga kuvifanya vyama vya upinzani vikose mawakala wa akiba iwapo itatokea dharura miongoni mwa wale walioapishwa, dharura zinazoweza kujitokeza ni kuumwa, kusafiri nje ya vituo, au kutekwa kabla ya kufika katika vituo vyao.

Iwapo mawakala hao watakosekana kwa dharura, baadhi ya vituo watabaki mawakala wa CCM pekee kwani hakutakuwa na mawakala wa akiba wa kuziba nafasi zao kwa kuwa ni lazima mawakala wawe wamekula viapo vya kisheria ili kupata uhalali wa kufanya kazi hiyo.

Reginald Munisi ameleza kuwa Chadema na Ukawa kiujumla wamejipanga vyema kuzikabili mbinu hizo chafu huku akiwaonya wale watakaoshiriki mipango hiyo kuachana nayo mara moja kwani tayari imefahamika na wanaweza kukumbana na nguvu ya Umma.

error: Content is protected !!