July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siri ya Polisi waliouana yabainika

Spread the love

SIRI ya askari polisi wawili waliofariki jijini hapa imefahamika baada ya kudaiwa kuwa wawili hao walikuwa wanakopeshana fedha za mishahara na posho zao za kila miezi miwili. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Inadaiwa kuwa marehemu aliyempiga risasi mwenzie kisha na yeye kujiuawa, PC Masunga Elisha, inadaiwa alimkopesha fedha zake za mshahara na posho za miezi miwili lakini mwenzake PC Petro Matiko, alishindwa kulipa kama walivyokubaliana.

Chanzo cha habari hizi kinaeleza kuwa PC Elisha alipokuwa akimuomba mwenzake fedha zake wakati muda wa kupeana pesa ulipowadia lakini PC Matiko alikuwa akipiga chenga kila wakati.

Pia inadaiwa kuwa baadhi ya askari polisi waliopo katika kambi ya polisi Mabatini jijini hapa, wamekuwa wakikopeshana fedha za mishahara na posho za miezi miwili na hukubaliana kupeana kadi ya benki kwenda kutoa fedha.

Aidha chanzo hicho kinaelezwa kwamba, hata hatua ya PC Elisha kufikia kufanya unyama huo imetokana na mwenzake kushindwa kufikia makubaliano yao waliokubaliana.

“Hata jana kama inavyoelezwa aliyepigwa risasi (marehemu Petro Matiko) alipotoka benki aliwaambia mtandao unasumbua, ndo maana sasa mwenzake aliona hakuna njia nyingine ya kufanya tofauti na kumpiga risasi,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina gazetini.

Mwili wa Matiko waagwa

Mwili wa marehemu, Petro Matiko, jana heshima zake za mwisho zilitolewa katika viwanja vya polisi Mabatini, Nyamagana mkoani hapa.

Heshima za mwisho za marehemu PC Matiko, ziliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga na maofisa wa jeshi la Polisi mkoani Mwanza.

Akiwasilisha salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, amesema kifo cha askari huyo kimekuja katika wakati ambao haukustahili kwani Taifa bado lilikuwa linamtegemea na familia yake kwa ujumla.

Afisa Mnadhimu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Japhet Lusingu, alitoa pole kwa familia ya marehemu sambamba na jeshi hilo mkoani hapa kwa kutoa ubani wa Sh. Milioni moja kwa baba mzazi wa marehemu.

Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyakato, Mrakibu Msaidizi, Almachius Muchunguzi, akisoma wasifu wa marehemu, amesema marehemu alizaliwa Machi 25 mwaka 1989, katika kijiji cha Nkende Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Hata hivyo mwili wa marehemu, PC Masunga Elisha, haukuagwa bila kutolewa kwa sababu za msingi ambazo hazikuwekwa bayana na uongozi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa.

error: Content is protected !!