October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simulizi ya Tundu Lissu ilivyosisimua

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

TUNDU Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ametoa simulizi ya hali aliyonayo sasa iliyowafanya wasikilizaji kulengwa lengwa na machozi na simanzi zikitawala. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Lissu ametoa simulizi hiyo leo Jumatatu tarehe 27 Julai 2020 mbele ya viongozi wa Chadema, ndugu jamaa na marafiki katika Ofisi za chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam

Mwanasiasa huyo, alikuwa anazungumza akiwa ofisini hapo akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam mara baada ya kuwasili akitoka nchini Ubelgiji.

Lissu alikuwa nje ya Tanzania tangu tarehe 7 Septemba 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na 16 zikimpata mwilini akiwa ndani ya gari kwenye makazi yake Area D jijini Dodoma.

Usiku huohuo, alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi na tarehe 6 Januari 2020 alihamishiwa Ubelgiji hadi aliporejea le Jumatatu.

Katika mazungumzo haye, Lissu mara kadhaa akisema ‘”Mungu ni mwema” amewashukuru Watanzania na wasio Watanzania kwa kujitoa kumgharamikia matibabu hadi akapona.

“Mungu wetu ni mwema sana, katika mazingira ya kawaida sikutakiwa niwe hai mpaka leo, nimerudi nyumbani kwetu, ni miaka mitatu kasoro mwezi ifike ile siku ambayo hata sikumbuki hata niliondokaje nchini, miaka mitatu ambayo ilikuwa ni migumu sana,” amesema Lissu

Huku ukimya ukiwa umetawa ukimsikiliza, Lissu amesema, “mkiniona nimevaa hivi unaweza usielewe sana, kungekuwa na uwezekano wa kuvua magwanda haya, wote mtakimbia kwa sababu huu mwili ukiachia kichwa na uso, huu mwili ni ramani za makovu ya risasi na visu vya Madaktari, huu mwili una vyuma vingi.”

Kauli hiyo iliwafanya wanaomsikiliza kuonyesha nyuso za majonzi na miongoni wakionekana kuchukua vitambaa vyao hususan wanawake kukijifuta usoni.

Lissu ambaye ni mtia nia ya Urais ndani ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, amesema mwaka huu utakuwa mgumu, hivyo wanachama wa Chadema wanatakiwa wajiandae na kujipanga.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi, mwaka wa kelele nyingi tofauti na miaka mingine ya kelele nyingi. Mwaka huu utakua mgumu kwelikweli tujiandae, anayefikiria itakua rahisi huyo hafahamu, hajaisoma namba kama ninavyosikia wanasema wanaisoma namba,” amesema Lissu.

error: Content is protected !!