July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simulizi msisimko majeruhi ajali ya ndege Mafia

Spread the love

HASSAN Bakari Ali, majeruhi wa ajali ya ndege iliyotokea Mafia wilayani Pwani, ameeleza kilichomtokea. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Ajali hiyo ilitokea Jumanne tarehe 6 Agosti 2019 wakati ndege hiyo inayofanya safari zake Mafia – Dar es Salaam – Mafia ilipoanza kupaa katika Uwanja wa Ndege wa Mafia uliopo kwenye eneo la Kilindoni.

“Ilikuwa tarehe 6 Agosti 2019, kwenye saa nne asubuhi hivi, nilikuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Tropical. Kwa kweli sikujua nini kilichosababisha ndege ile kushindwa kuruka zaidi ya mita mbili kutoka chini,” amesema.

Hassan ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mafia, kwa sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), akipatiwa matibabu.

Amesema, ndege hiyo iliruka kwa mita zisizozidi tano na kusababisha kugonga ukuta wa nyaya uliozunguka uwanja huo, ndipo ikaanguka na kuanza kuwaka moto.

Hassan ameeleza, alikuwa amekaa karibu na mlango wa nyuma wa ndege hiyo ambao ndio ulioanza kuwaka moto.

Na kwamba, rubani wa ndege hiyo alifanikiwa kufungua milango ya mbele hiyo ikiwa ni hatua za awali kusaidia kuogoa abiria wake.

Majuruhi huyo anaeleza, alikuwa nyuma wakati huo ndege hiyo imeanza kuwaka moto, kutokana na mazingira magumu ya ndani humo, alitafuta namna ya kujiokoa kwa haraka.

Ndipo alipoona nyuma kuna nafasi ya kupita licha ya kuwa moto ulikuwa unakolea ‘niliamua kupita hapo hapo, sikujali moto uliokuwa unawaka kwenye mlango huo.’

Hassana anasema, kwa wakati huo yeye na wenzake tisa akiwemo rubani, kila mmoja alikuwa akihaha namna ya kujiokoa.

Na kwamba, hakuona namna nyingine isipokuwa kupita katikati ya moto huo kwenda nje ya ndege hiyo.

“Kweli moto ulikuwa umewaka lakini akili yangu haikuona njia nyingine isipokuwa kwenye mlango ambao moto ulikuwa unakolea,”amesema na kuongeza;

“Nilifanikiwa kupenya katikati ya moto mpaka nje, ndio nikagundua kwamba tayari nilikuwa nimeanza kuungua,” amesema.

Huku akionesha baadhi ya majeraha yake Hassan anasema, mvuke wa moto umemwathiri zaidi kwenye usoni, kifuani, mikononi na miguuni.

“Daktari amesema nimeungua lakini sina majeraha ya ndani kutokana na moto ule,” ameeleza.

Akizungumzia vitu vya thamani alivyokuwa navyo, amesema amepoteza kompyuta mpakato (Laptop), simu na nyaraka zake za biashara.

error: Content is protected !!