December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Simulizi magaidi waliotoroka gerezani walivyonaswa kininja, njaa imewaponza

Spread the love

 

MAGAIDI watatu walionaswa kichakani katika kijiji cha Kamuluyuni kilichoko kaunti ya Kitui nchini Kenya  baada ya kutoroka gereza la Kamiti, walijaribu kuwahonga polisi wa akiba waliowafumania mafichoni. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Kwa mujibu wa magaidi hao Musharaf Abdallah Akhuluya, Joseph Juma Odhiambo na Mohamed Ali Abikar, waliwahonga walinzi wa gereza la Kamiti wakafunguliwa lango kuu na kutoroka.

Magaidi hao walikamatwa tarehe 18 Novemba mwaka huu walipokuwa wamepumzika kijijini hapo baada ya kutembea umbali mrefu kutoka Gereza la Kamiti na wakipitia Kaunti ya Machakos na kuchapa mwendo hadi Kitui.

Watatu hao walilenga kuingia kwenye msitu ulio karibu na mji mdogo wa Endau ambao upo ndani ya Kenya na Somalia.

Inaelezwa kuwa walipofika katika eneo la Kamuluyuni, simu waliyokuwa nayo iliishiwa chaji na kuzidiwa uchovu pamoja na njaa.

Akizimulia tukio hilo, Petero Komu Kilonzi ambaye ni polisi wa akiba katika eneo hilo alisema Jumatano jioni tarehe 17 Novemba, alipewa taarifa na wakazi wa eneo hilo kwamba, waliona watu waliowashuku wakitembea kati ya Kamuluyuni na msitu wa Endau.

Kilonzi alichukua walinzi wenzake na kuelekea hadi Endao kujionea kilichokuwa kikiendelea katika msitu huo.

Kilonzi aliyejitwika majukumu ya kuwa polisi wa akiba (APR) mwaka 2017, siku iliyofuata akiwa na wenzake 15 walirudi msituni lakini ilipofika saa nne asubuhi, walirudi katika eneo la Kamuluyuni.

Walipowasili katika soko la Kamuluyuni, Kilonzi alipaki pikipiki yake na kuzunguka kijijini hapo akiuliza wakazi iwapo walikuwa wamewaona watu waliowashuku.

Afisa huyo wa APR alikutana na mwanamke aliyemwambia kwamba, aliona mwanamume aliyekuja nyumbani kwake kuomba chakula.

Mwanamke huyo alisema alimpakulia ‘githeri’ chakula maarufu cha nchini humo, alichobeba na kumpelekea mwenzake aliyekuwa amejificha nyuma ya ua.

Huku wakiendelea na mazungumzo, Kilonzi aliona mtu amejificha kichakani na kumwendea mwanamume huyo ambaye baadaye ilibainika kwamba alikuwa Musharaf Abdalla Akhulunga, aliyehukumiwa kifungo baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kulipua majengo ya Bunge mnamo 2012.

Huku wakiendelea kuzungumza, Kilonzi ghafla alimrukia na kujaribu kumfunga pingu. Lakini Musharaf alikwepa na kuanza kumshambulia Kilonzi.

Baada ya kupambana kwa muda, Kilonzi alimzidi gaidi huyo na kumfunga pingu.

Baadaye, Kilonzi pamoja na watu waliofika kumsaidia, walimbeba gaidi huyo na kumweka juu ya pikipiki na kisha kumpeleka katika eneo la soko.

Musharaf alipofika huko, aliomba maji na chakula ambapo Kilonzi alimnunulia chapati na maharage.

Baadhi ya maafisa wa APR walikimbilia msituni na baada ya muda mfupi, waliwanasa Abikar na Odhiambo.

Waliwaketisha karibu na Musharaf na kuanza kuwahoji lakini cha ajabu mmoja wa wafungwa hao wa ugaid aliyefahamika kwa jina la Abikar alianza kupiga mayowe huku akiwasihi maafisa hao wa APR wawaue kwa risasi kuliko kuwarejesha gerezani Kamiti.

Abikar alihukumiwa kifungo baada ya kupatikana hatia ya kuhusika na shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa ambapo watu 148 waliuawa mnamo 2014 na kuhukumiwa kifungo cha miaka 41 gerezani.

Abikar aliwataka maafisa wa APR wakubali kuchukua hongo ili wawaachilie huru.

Maafisa wa APR waliwasiliana na polisi wa Kituo cha Nuu ambao walifika katika eneo hilo baada ya muda mfupi.

Odhiambo aliyefungwa kwa kujaribu kujiunga na kundi la wapiganaji la al-Shabaab mnamo 2019, hakutamka neno wakati huo wote.

Walipofikishwa katika Kituo cha Polisi cha Nuu, Abikar alikiri kwamba hawakupanda ukutani kama ilivyodaiwa.

Alifichua kuwa walifunguliwa lango kuu na walinzi wa gereza wakaondoka.

Maafisa wakuu wa gereza la Kamiti tayari wamekamatwa na wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka  tarehe 16 Novemba 2021.

Pia Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimtimua kazi Kamishna Jenerali wa Magereza nchini humo, Wycliffe Ogallo baada ya wafungwa hao kutoroka tarehe 15 Novemba mwaka huu.

Serikali ya Kenya ilikuwa imetangaza donge nono la Sh bilioni 1.2 kwa mtu yeyote ambaye angetoa taarifa kwa magaidi hao kukamatwa

error: Content is protected !!