January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simbachawene awabana wakandarasi

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene

Spread the love

WAZIRI wa Nishati na Madini, George Simbachawene amewaagiza wakandarasi wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Kigoma, kuhakikisha wanasimamisha nguzo za umeme kabla ya Juni 30, mwaka huu. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Simbachawene alitoa agizo hilo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) ambaye alilalamikia kusuasua kwa utekelezaji miradi ya umeme katika mkoa huo.

Amesema utekelezaji wa miradi ya umeme katika mkoa huo kwa sasa ni asilimia 40 tu na kwamba maeneo mengi nguzo zimelazwa lakini hakuna kazi yoyote inayoendelea.

“Ni kweli miradi ya REA Kigoma inasuasua kwa kuwa kasi yake siyo nzuri, nilishakutana na wakandarasi nikaawagiza wahakikishe wamesimamisha nguzo za umeme ifikapo Juni 30 mwaka huu.

“Mkandarasi ambaye atakutwa bado amelaza nguzo chini tutamchukulia hatua,” amesema Simbachawene.
Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), Simbachawene amesema serikali kupitia Shirika la Umeme (Tanesco), imefanya tathmini ya kazi ya kufikisha umeme katika Tarafa ya Nguruka.

“Vijiji vya tarafa hiyo havikujumuishwa kwenye Mpango Kabambe wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili chini ya ufadhili wa Mfuko wa Nishati Vijijini (REA) kutokana na ufinyu wa bajeti.

“Hata hivyo, vijiji hivyo vitapewa kipaumbele katika miradi ya  Umeme Vijijini (REA) ya kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu,” amesema.

Katika swali lake, Kafulila alitaka kujua lini serikali itafikisha umeme katika Tarafa ya Nguruka wilayani Uvinza.

error: Content is protected !!