July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simbachawene atimua maofisa biashara Dodoma

Spread the love

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene amewasimamisha kazi Maofisa Biashara wa Mkoa wa Dodoma kutokana na kosa la urasimu katika utoaji wa leseni za biashara. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Mjini hapa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka ofisi ya Rais (Tamisemi), Rebeca Kwandu amesema waliosimamishwa kazi ni Elias Kamara na Donatila Vedasto.

“Agizo hili limetolewa na Waziri baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara ambao ilionesha kuwepo kwa mazingira ya rushwa katika utoaji wa leseni za biashara,’’ amesema Kwandu.

Amesema katika uchunguzi huo uliofanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imegundua kuwa kulikuwa na maombi ya leseni 750 ambayo hayajashughulikiwa bila ya sababu za msingi.

Pia amesema hali hiyo imeisababishia kuikosesha Manispaa ya Dodoma mapato ya Sh.75 milioni hali ambayo imerudisha nyuma uchumi wa mkoa.

Amesema  Simbachawene alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kujaza nafasi hizo kwa kukaimisha watu wenye sifa ili waweze kufanya kazi hizo.

Aidha Kwandu amesema pia Waziri huyo ameagiza Mamlaka za Serikali kuhakikisha wanatoa leseni za biashara bila urasimu wowote.

“Nawaomba wanaohusika kutoa leseni kwa wahusika na wapatiwe ndani ya siku mbili au tatu, pamoja na kuacha urasimu katika kutoa leseni na kujiepusha na vitendo vya rushwa,’’ amesema Kwandu kwa niaba ya Waziri.

error: Content is protected !!