January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simbachawene apuuza tuhuma kuuzwa gesi ya Mtwara

Spread the love

WAZIRI wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesema, taarifa za kuuzwa kwa gesi ya Mtwara hazina ukweli wowote. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Kauli hiyo inatokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai, gesi iliyogunduliwa mkoani Mtwara imeuzwa kwa wawekezaji.

Simbachawene amesema hayo leo ofisini kwake Jijini Dar es Salaam wakati akiaga wanafunzi 22 wa vyuo vikuu ambao wamedhaminiwa kwenda nchini China kwa miaka mitatu kusomea masuala ya gesi na mafuta.

“Gesi haijauzwa na wala hakuna muwekezaji aliyesaini mikataba na mikataba yenyewe bado haijakamilika, ndio kwanza tunatengeneza,” amesema na kuongeza “wananchi na baadhi ya viongozi waache kuongea uongo bali wafanye uchunguzi.”

Hata hivyo amesema, gesi iliyogunduliwa nchini mpaka sasa haijaanza kuuza mahali popote duniani.

“Gesi tuliyonayo bado haijaaza kuuzwa popote na tuliyonayo kwa sasa ndo hiyo ya kutoka Mtwara ambayo inatumika kutengenezea umeme na matumizi mengine.

“Tayari tunamiliki bomba kubwa la gesi linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam,” amesema.

Akizungumzia wanavyuo hao amesema, wamedhaminiwa na Serikali ya China kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Madini.

Simbachawene amesema, msaada huo hutolewa na Serikali ya China kila mwaka ambapo waliaza mwaka 2013 na kuchukua wanafunzi wanane, mwaka 2014 walichukua wanafunzi 10 ambapo mwaka huu wamechukua 22.

Awali, wanafunzi waliojitokeza kuomba nafasi hiyo walikuwa 187 na baada ya mchujo walipatikana 33.

Hatua iliyofata anasema, walipeleka majina hayo kwenye Ubalozi wa China ambapo nao walichuja majina hayo na kubaki wanafunzi 22 kulingana na vigezo walivyoweka.

Mgawanyo wa wanafunzi hao ni kuwa, watatu kati ya 22 ambapo wote ni wanaume watasomea Shahada ya Uzamivu kuhusu mafuta na gesi.

Waliobaki ambao ni wanawake wanane na wanaume 11 watasomea Shahada ya Uzamili.

“Lengo la kuwapeleka wanafunzi wao wa elimu ya juu ni kupata uelewa zaidi wa masuala ya mafuta na gesi ili wakirudi walete maendeleo nchini,” amesema.

Pia Simbachawene amewataka wanafunzi hao warejee Tanzania mara baada ya kuhitimu masomo yao ili kusaidia changamoto zinazoikabili Wizara na Taifa nzima.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuendeleza sekta ndogo za ya gesi asilia, kuanzisha vyanzo mbadala vya nishati ya umeme badala ya kutegemea maji.

Changamoto nyingine ni kuongeza usimamizi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya gesi asilia, kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji, kudhibiti changamoto za upotevu wa umeme wakati wa kusafurisha.

“Kama mnavyoelewa, wizara hii ni miongoni mwa wizara zilizopo katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), na ili kutekeleza ipasavyo wanahitajika wataalamu wazalendo waliobobea katika fani za mafuta na gesi asilia.

“Ni matumaini yangu kuwa, mtaitumia fursa hii vizuri kwa kujifunza yaliyo mazuri pia kwa namna ya pekee niishukuru Serikali ya China kwa msaada huu wa kuwaendeleza Watanzania ambapo wamesema mpango huu upo hadi mwaka 2019.” amesema Simbachawene.

error: Content is protected !!