July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simbachawene amkubali mbaya wa Prof. Muhongo

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo akimkabidhi ofisi waziri mpya wa wizara hiyo, George Simbachawene

Spread the love

WAZIRI mpya wa Nishati na Madini, George Simbachawene amekabidhiwa rasmi ofisi na harakaharaka akatambua mchango wa Dk.   Reginald Mengi, ambaye alikuwa adui mkubwa kwa mtangulizi wake Profesa Sospeter Muhongo. Anaripoti Sarafina Lidwino.

Simbachawene, mwanasheria kitaaluma, alikabidhiwa ofisi leo mchana ikiwa ni wiki moja tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.

Mbunge huyu wa Kibakwe, mkoani Dodoma, aliwahi kuwa naibu waziri katika wizara hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Makabidhiano ya ofisi yalifanywa kwa Profesa Muhongo kutoa maelezo mafupi akisema, “… ninayo imani kubwa sana na uadilifu, uaminifu na utendaji wako. Na imani utaendelea kuweka maslahi ya Watanzania wote hasa maskini na wanyonge juu ya maamuzi yako, busara na hekima zako zitaendelea kuimarisha majukumu ya wizara kwa ustawi wa taifa letu.”

Profesa Muhongo alijiuzulu uwaziri kwa shinikizo la Bunge na umma baada ya kuhusishwa na kutowajibika katika kashfa ya kuchotwa kwa zaidi ya Sh. 300 bilioni zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, iliyohifadhiwa fedha zilizotokana na mgogoro wa utekelezaji wa mkataba wa kufua umeme kati ya Tanesco na IPTL.

Kwa muda wote aliokuwa waziri wa nishati na madini, Prof. Muhongo ambaye ni mtaalamu mbobezi wa miamba, alijenga na kuwa katika mvutano mkali na wafanyabiashara wa Tanzania hususani kiongozi wao kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi (PSPF), Reginal Mengi.

Mara kadhaa Profesa Muhongo alijibizana maneno ya kejeli, vijembe na hata dharau akimlenga Mengi, ambaye ni mwenye msimamo kwamba serikali inao wajibu wa kushirikiana na wafanyabiashara wazawa ili watumie fursa ya kuwekeza katika sekta ya utafiti na uchimbaji gesi.

Wakati fulani Prof. Muhongo alisema wafanyabiashara nchini hawana uwezo wa kuwekeza kwenye gesi kutokana na gharama kubwa kimtaji, badala yake uwezo walionao ni “pesa za kununulia juisi tu.”

Lakini leo, Mengi alipewa nafasi maalum na waziri mpya Simbachawene, ya kuzungumza hata maneno machache, mbele ya vyombo vya habari kama hatua ya kile alichoita, “natambua kuwepo kwa mheshimiwa Mengi, una machache ya kuzungumza, karibu tafadhali.”

Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, ambaye alipofika ukumbini Prof. Muhongo alikuwa ameshaondoka, alisema, kwa nafasi yake ndani ya asasi ya sekta binafsi, anamuahidi ushirikiano mkubwa.

“Nitakuwa nawe bega kwa bega na kama kuna tatizo lolote usisite kuniambia kwa sababu lengo ni Watanzania na taifa letu kufaidika na utendaji wako,” alisema.

Katika hafla hiyo, Waziri Simbachawene alitangaza rasmi kusudio la kuuzwa kwa hisa za mradi wa madini ya Nickel wa Kabanga, wilayani Ngara.

Alisema wizara inapenda kujulisha umma kwamba kampuni za nchini Canada za Glencore na Barrick Gold zinauza hisa kwa wananchi katika mradi huo wa Nickel.

“Baada ya kufuatilia kwa makini bei ya madini ya Nickel kwenye soko la dunia na ushindani mkubwa wa mitaji adimu kwa bidhaa mbalimbali, kampuni ambazo ni wanahisa kwenye mradi zinaanza mchakato wa kuuza hisa zao kwa pamoja,” alisema.

Alisema mradi huo una thamani kubwa na timu ya wafanyakazi mahiri ukishikwa na wanahisa wenye mahusiano mazuri na Wizara, Serikali za Mitaa na jamii inayozunguka mradi pamoja na wadau wengine muhimu.

“Hawa wamesaidia uwekezaji kuundeleza mradi wenye thamani ya Dola zaidi ya milioni 264 katika muongo uliopita. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kuongeza mashapo hadi kufikia tani milioni 58.2 zenye asilimia 2.6 ya metali ya nikeli na hivyo kuufanya mradi wa Kabanga Nickel kuwa na mashapo makubwa kidunia,” inasema taarifa ya Waziri Simbachawene.

Kampuni ya Kabanga Nickel ambayo imeajiri wafanyakazi 55 na wakandarasi, ina ofisi jijini Dar es Salaam na kambi ya utafutaji madini na inaingiza maduhuli ya pango la leseni ya takriban Dola 434,000.

“Tutahakikisha kuwa maslahi ya taifa na jamii inayozunguka mradi yanalindwa wakati huu na baada ya mchakato wa mauzo ya hisa,” alisema Waziri Simbachawene.

Katika utendaji wake, anasaidiwa na manaibu wawili ambao ni Steven Maselle, waliyekuwa pamoja kabla kama manaibu chini ya Prof. Muhongo, na Charles Mwijage aliyepata uteuzi kwa mara ya kwanza.

error: Content is protected !!