July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simbachawene afanya ziara ya kushitukiza S/msingi

Spread the love

WAZIRI  wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene amefanya ziara ya kushutukiza katika shule ya msingi Dodoma Makulu katika manispaa ya Dodoma baada ya kubaini mkuu wa shule ameitisha wazazi kwa kutaka wachangie. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Hali hiyo ilionekana kumkera Waziri kutokana na mkuu wa shule hiyo Janethi Justine kukiuka waraka wa  Serikali  wa elimu bure kuanzia awali hadi kidato cha nne.

Suala hilo limekuwa kizungumkuti kufuatia Ofisa Elimu shule ya Msingi wa manispaa ya Dodoma, Scola Kapinga kuandika barua kwa shule za msingi katika manispaa yake mkoani hapa kuzitaka kuchangisha michango mbalimbali.

Hali hiyo kumepelekea Simbachawene akiambatana na Naibu katibu mkuu Tamisemi Elimu, Bernard Makali kufanya ziara ya kushtukiza katika shule hiyo ilo  kujionea hali halisi ya mgawanyo wa fedha za elimu bure huku wazazi wakichangishwa .

Waziri huyo akizungumza na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Janeth Justine alimuhoji kuhusiana na uendeshaji wa elimu katika shule hiyo pamoja na kutaka kujua idadi ya wanafunzi.

Mwalimu huyo alijibu kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,400 na ilipokea fedha za elimu bure jumla ya Sh. 152,000 milioni na walizigawanya fedha hizo kulingana na waraka namba 6 wa serikali.

“Asilimia 30 vifaa, asilimia 30 ukarabati, mitihani asilimia 20 ambapo kwenye michezo ni asilimia 10 huku utawala ni asilimia 10 lakini pia nilipokea barua toka Manispaa ikielekeza kuwachangisha wazazi fedha za mlinzi, umeme na maji.

“Nilivyopokea barua niliitisha kikao jana cha wazazi (juzi) ambapo wazungumzaji alikuwa diwani wa Kata hiyo, Paschal Matula aliwataka wazazi kukubaliana kutoa michango hiyo mlinzi Sh. 50,000, Maji Sh. 72,000 na umeme kiasi cha Sh 150,000 kwa mwaka,” amesema Mwalimu Janeth.

Hata hivyo amesema kuwa katika kikao hicho hawakufikia muafaka baada ya wazazi kuweka mgomo juu ya kuchangia michango hiyo.

Kufuatia kuwepo kwa michango hiyo Waziri huyo alitoa agizo kwa Wakurugenzi, wakuu wa Wilaya na wakuu wa mikoa nchini kusoma vizuri waraka namba 6 uliotolewa na Serikali kuhusu mchanganuo wa elimu bure na kuacha kuchangisha michango wazazi isiyokuwa ya lazima.

“Inaonekana kuna watu wanataka kujinufaisha na michango hiyo kupitia wazazi kwani michango ambayo wazazi walikuwa wanatakiwa kuchanga tayari serikali ilishalipa michango yote na walimu wakuu walishakabidhiwa,” amesema Simbachawene.

Awali akielezea kuhusu fedha ambazo zimetolewa na serikali za elimu bure Waziri Simbachawene amesema kuwa Serikali imepanga kutoa fedha hizo kila mwezi tofauti na walimu wanavyofikiria kuwa fedha walizopatiwa ni za mwaka mzima.

Waziri huyo alifafanua kuwa mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi amelipiwa kiasi cha Sh. 548 huku kwa mwanafunzi wa sekondari kutwa amelipiwa kiasi cha 3,540 ambapo kwa wanafunzi wa sekondari wa bweni wao wanalipiwa Sh 7,243.

Amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya Sh. 18.77 bilioni kwa ajili ya shule hizo kwa kila mwezi ambapo kwa miezi sita hadi Julai mwaka huu imetenga jumla ya Sh. 131 bilioni.

Fedha hizo ni  kwa ajili ya matumizi ya utendaji wa shule ikiwemo umeme, maji malipo ya mlinzi, ada, gharama za mitihani pamoja na chakula kwa wanafunzi wa bweni.

error: Content is protected !!