December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Simba yazisomba tuzo za TFF, Yanga kiduchu

Spread the love

TIMU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imejizoelea tuzo kibao za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) huku watani zao wakiambulia ‘kiduchu.’ Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tuzo hizo zimetolewa usiku wa kumkia leo Ijumaa, tarehe 22 Oktoba 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi kwenye tuzo hizo za Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wachezaji wa Simba waliotwaa tuzo ni; Aishi Manula aliyetwaa ya kipa bora wa ligi kuu msimu wa tano mfululizo pamoja na kipa bora wa kombe la shirikisho.

Nahodha wa kikosi hicho, John Bocco ametwaa tuzo ya mfungaji bora na mchezaji bora wa ligi Kuu (MVP) msimu wa 2020/21.

Pia, Mohamed Hussein yeye ametwaa tuzo ya beki bora akiwashinda Dickson Job wa Yanga pamoja na Shomari Kapombe wa Simba.

Waliokuwa wachezaji wa Simba msimu huo, Clotous Chama ametwaa tuzo ya kiungo bora. Kwa sasa Chama anakipiga Berkane ya Morocco aliyejiunga nao msimu huu.

Pia, Didier Gomes wa Simba, ametwaa tuzo ya kocha bora wa msimu 2020/21. Amewashinda George Lwandamina wa Azam FC na Francis Baraza wa Kagera Sugar, ambaye alijiunga na Kagera akitokea Biashara United ya Mara.

Feisal Salum ‘Fei Toto’ akipokea tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la Shirikisho kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Wachezaji wa Yanga waliotwaa tuzo ni wawili pekee, beki Shomari Kibwana aliyetwaa tuzo ya ‘Fair Ply’ baada ya kuonesha mchezo wa kiungwana katika moja ya mechi, baada ya kuchezawa faulo na hakuonekana kuchukizwa.

Mwingine ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye kwa sasa yuko kwenye kiwango cha juu, ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho.

Katika kuonesha Simba ilikuwa bora msimu uliopita, kwenye kikosi cha wachezaji 11, imeingiza wachezaji saba huku Yanga ikiwa na wachezaji watatu na Azam akiingia Prince Dube kama mshambuliaji.

Kikosi hicho, kiko chini ya Nahodha John Bocco.

Kikosi chote na namba zao kwenye mabano ni kipa Aisha Manula, Shomari Kapombe (2), Mohamed Hussein (3), Joshia Onyango (4), Clotous Chama (7), John Bocco (10) na Louis Miquisson (11) wote wa Simba.

Wengine ni, Dickson Job (5), Mkoko Tunombe (6), Feisal Salum ‘Fei Toto’ (8)wote Yanga, Prince Dube (9) wa Azam FC.

error: Content is protected !!