May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba yatangaza michuano yake, kocha mpya…

Barbara Gonzalez, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba

Spread the love

 

TIMU ya Simba ya Dar es Salaam, imetangaza michuano ya Kimataifa ‘Simba Super CUP’ ikihusisha timu tatu Simba, TP Mazembe ya Congo na Al Hilal ya Sudan. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, timu hiyo imesema, kesho Jumamosi, itamtangaza kocha mpya atakayechukua mikoba ya Sven Vanderbroeck aliyeondoka. Kocha mpya atasaidiwa na kocha msaidizi, Suleiman Matola.

Akitangaza michuano hiyo leo Ijumaa tarehe 22 Januari 2021, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba (CEO), Barbara Gonzalez amesema, michuano hiyo, itaanza Jumatano ijayo tarehe 27- 31 Januari 2021.

Amesema, mechi ya kwanza itakuwa Simba dhidi ya Al Hilal saa 11 jioni.

Haji Manara, Ofisa Habari wa Klabu ya Simba

Msemaji wa Simba, Haji Manara amesema, michuano hiyo “ni maalum kwa mabingwa wa nchi, kama timu yako siyo bingwa, huhusiki na michuano hii.”

“Lakini, michuano hii ni maalum kwa maandalizi ya michuano ya klabu bingwa, tunataka kushinda kikombe,” amesema Manara

Amesema, kabla ya michuano hiyo kuanza, benchi lote la ufundi litakuwa limekamilika na “kuanzia kesho, tutaanza kutangaza kocha na benchi lake la Ufundi.”

“Ndani ya siku mbili au tatu zijazo, tutakuwa na kocha mkuu mpya atakayesaidiana na Suleiman Matola,” amesema Manara

Manara amesema, “malengo yetu kimataifa ni kufikia nusu fainali, lakini malengo yetu mama ni kushinda ligi kuu na kombe la FA.”

error: Content is protected !!