April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Simba yanusa robo fainali, As Vital yapigwa

Spread the love

 

SAFARI ya timu ya Simba ya Tanzania, katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, imeshika kasi, baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0, dhidi ya El Merrikh ya Sudan. Anaripoti Klevin Mwaipungu…(endelea).

Simba imeibuka na ushindi huo leo Jumanne, tarehe 16 Machi 2021, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, nchini Tanzania.

Ushindi huo, umewafanya Simba kufikisha pointi 10 na kuendelea kuongoza kundi A ikifuatiliwa na Al Ahly ya Misiri yenye pointi saba, baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya AS Vital ya Congo.

As Vital imepoteza mchezo huo uliochezwa nchini Congo na kuwafanya kubaki na pointi nne nafasi ya tatu na El Merrikh ikisalia na alama mbili.

Katika mchezo wa leo, Simba ilianza kuhesabu kalamu ya magoli dakika ya 18, kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Lous Miquisonne, baada ya kuwashinda ujanja mabeki ya El Merrikh.

Dakika ya 39, beki kitasa wa Simba, Mohamed Hussein, alipokea pasi maridadi kutoka kwa Bernard Morrison na mabeki we El Merrikh wakidhani Hussein ameotea, aliachia shuti kali, lililokwenda moja kwa moja nyavuni.

Timu hizo, zilikwenda mapumziko kwa Simba ikiwa mbele kwa magoli 2-0 huku ikishuhudia beki wake wa kati, Josash Onyango, akitoka dakika ya 45, baada ya kuumia na nafasi yake, kuchukuliwa na Erasto Nyoni.

Vinara hao wa Kundi A, walirejea kipindi cha pili kwa kasi kwa kuliandama goli la Merrikh na iliwachukua dakika tatu za kipindi cha pili kujipatia goli dakika ya 48, kupitia kwa Chris Mugalu, aliyepokea pasi ya Lous Miquisonne.

Katika dakika zote 90 za mchezo, Simba ilicheza kandanda safi na la kuvutia kwenye uwanja wake wa nyumbani ambao haukuwa na mashabiki, kutokana na zuio lililotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Zuio hilo, lilitokana na kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

Kwa sasa, Simba inahitaji pointi moja kati ya michezo miwili iliyosalia dhidi ya As Vital utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na ule wa Al Ahly, utakaochezwa Misiri.

error: Content is protected !!