January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba, Yanga zategana

Spread the love

 

ZIKIWA zimebaki siku nne, kuelekea kupigwa kwa pambani la watani wa jadi kati ya Simba ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo dhidi ya Yanga, mafahari hao wawili kwenye soka la Tanzania kila pande imeonesha nia ya kutaka kushinda mchezo huo ili kujiwekea mazingira mazuri katika safari za mbio za Ubingwa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utapigwa siku ya Jumamosi, Disemba 11, mwaka huu majira ya saa 10 jioni kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Umuhimu wa mchezo huo kwa timu zote unakuja kutokana na msimamo wa Ligi ulivyo mpaka sasa mara baada ya kupigwa michezo saba katika duru hili la kwanza toka kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22.

Yanga kwa sasa ipo kileleni ikiwa na pointi 19, huku Simba ikiwa nafasi ya pili wakiwa na pointi 17, kama Yanga ikifanikiwa kushinda mchezo huo itazidi kujikita kileleni na kujitengenezea wigo mkubwa wa pointi dhidi ya mshindani wake wa karibu ambao ni Simba.

Kwa upande wa Simba ambao wana pointi 17, wanauhitaji mkubwa wa mchezo huo na kutaka alama tatu ambazo kama wakizipata kwa kuibuka na ushindi dhidi ya watani wao, watapaa kileleni kwenye msimamo na kuwa vinara wa Ligi hiyo kwa mara ya kwanza toka kuanza kwa msimu huu mpya wa kimashindano.

Simba inaingia kwenye mchezo huo, huku ikiwa imetoka nchini Zambia kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Red Arrows na kupoteza mchezo huo kwa mabao 2-1, lakini walifanikiwa kusonga mbele kutokana na uwiano mzuri wa mabao (Aggregate) katika michezo yote miwili .

Umuhimu wa mchezo huo hautaishia hapo tu, bali mpaka timu hizo mbili zinakwenda kukutana siku hiyo, hakuna hata mmoja kati yao aliyepoteza mchezo wowote kwenye Ligi kuu baada ya kupigwa mechi saba.

Katika michezo saba waliocheza Yanga mpaka sasa wamefanikiwa kushinda michezo sita na kwenda sare kwenye mchezo mmoja tu, ambao ni dhidi ya Namungo uliopigwa Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Kwa upande wa Simba, katika michezo saba waliocheza mpaka sasa wamepata ushindi kwenye mchezo mitano na kwenda sare michezo miwili dhidi ya Biashara United na Coastal Union.

Katika mchezo waliokutana mara ya mwisho 25 Septemba 2021 Kwenye ufunguzi wa Ligi (Ngao ya Hisani) Simba alipoteza kwa bao 1-0, mbele ya Yanga, bao lililofungwa na Fiston Mayele ambaye ni ingizo jipya katika msimu huu kwa upande wa Yanga.

Mara ya mwisho Simba kuibuka na ushindi mbele ya Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa msimu wa 2018/19, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, mchezo uliopigwa Februari 16, 2019.

Kwa upande wa Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Simba katika misimu miwili mfululizo kuanzia 2019/20 na 2020/21.

error: Content is protected !!