January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba, Yanga kucharuana usajili wa Okwi

Emmanuel Okwi akitambulishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zackaria Hanspoppe mara baada ya mshambuliaji huyo kusaini mkataba wa miezo sita

Spread the love

MADHARA ya kujaza wanachama na viongozi wa klabu za Simba na Yanga katika kamati mbalimbali za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa yanaanza kuonekana.

Jamal Malinzi, Rais wa TFF, alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, alikosolewa kwa hatua yake ya kuingiza marafiki, watu kutoka mkoa wa Kagera na wapenzi wa Simba na Yanga. Hakubadili kamati akidai kwamba alizingatia weledi.

Wiki hii, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliyosheheni wapenzi, viongozi wa zamani na sasa wa Simba na Yanga inatarajiwa kutoa uamuzi juu ya hatima ya kisoka ya Mganda Emmanuel Okwi, mshambuliaji aliyemwaga wino Msimbazi huku akiwa bado ana mkataba na Yanga.

Kamati hiyo ina wajumbe saba. Mwenyekiti ni Richard Sinamtwa; makamu wake ni  Moses Karuwa; na wajumbe ni Zacharia Hanspoppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega.

Kamati hiyo ina wapenzi wanne wa Yanga ambao ni Sauko (aliwahi kuwa mjumbe), Madega (aliwahi kuwa mwenyekiti) huku wapenzi wengine wakiwa Karuwa na Ntahilaja. Wapenzi wa Simba ni Sinamtwa, Mwamba na Hanspoppe, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, kiongozi aliyefanikisha usajili wa Okwi.

Kamati hiyo, ndiyo iliyobebeshwa ‘zigo’ hili kwa kuzingatia kanuni za usajili wa kimataifa na Ligi Kuu ya Vodacom. Wajumbe watacharuana kuhusu uhalali wa usajili wake Yanga na ubatili wake Simba au uhalali wake Simba na ubatili wake Yanga.

Hata hivyo, katika kanuni za usajili wa wachezaji, hakuna kupiga kura ila hoja na kanuni. Kwa hiyo wingi wa wapenzi wa Yanga hauna tija. Kinachoangaliwa ni uhalali wa mikataba na fomu za usajili basi.

Mchezaji anayeutia aibu mpira wa miguu kwa kujisajili klabu mbili huadhibiwa. Katika hili, TFF itakuwa msaada mkubwa kwani itaeleza mkataba uliopo ni wa kati ya Okwi na Yanga au Okwi na Simba.

Kanuni ya 55 kuhusu usajili inasema; “Haitaruhusiwa kwa mchezaji yeyote kutia saini mikataba ya klabu zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Mchezaji atakayesaini mikataba ya timu mbili tofauti kwa wakati mmoja, ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 43 (5).

Kanuni ya 43 (3) inasema; “Klabu inayotarajia kuingia mkataba na mchezaji wa kulipwa haina budi kuiarifu klabu yake ya sasa kwa maandishi kabla ya kufanya makubaliano na mchezaji huyo wa kulipwa. Mchezaji wa kulipwa atakuwa huru tu kuingia mkataba na klabu nyingine iwapo mkataba wake na klabu yake ya sasa umekwisha au utakwisha baada ya miezi sita. Uvunjaji wowote wa sharti hili utastahili vikwazo vinavyofaa.”

Lakini kanuni ya 43 (5) inasema; “Iwapo mchezaji wa kulipwa ataingia katika mkataba zaidi ya mmoja unaohusu kipindi kimoja, masharti yaliyowekwa katika Sura ya IV ya kanuni za FIFA yatatumika.”

Kanuni ya 13 katika Sura ya IV ya kanuni za FIFA inasema; “Mkataba kati ya klabu na mchezaji utasitishwa ama kwa makubaliano ya pande mbili au mchezaji kumaliza muda wa kuitumikia klabu.

Kanuni ya 16 inasema; “Mkataba hauwezi kuvunjwa katikati ya msimu wa ligi.”

Kanuni ya 17 (1) inayozungumzia madhara ya kusitisha mkataba bila sababu za msingi inasema; “Katika mazingira yoyote yawayo, upande wowote unaokiuka mkataba bila sababu za msingi utaadhibiwa kwa kulipa fidia.”

Kwa ufafanuzi huu wa kanuni, Okwi pamoja na klabu iliyomsaidia kukiuka mkataba wataaadhibiwa.

error: Content is protected !!