May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba yala kiporo, yaisogelea Yanga

Spread the love

 

USHINDI wa mabao 2-1, dhidi ya Dodoma jiji FC, umeifanya Simba kuondoka na pointi tatu muhimu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea)

Simba imeshinda mchezo huo leo Alhamisi tarehe 4 Februari 2021, na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Dodoma Jiji FC kwenye Uwanja wao wa nyumbani toka kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21.

Kabla ya mchezo huo, Dodoma Jiji ilikuwa imecheza michezo saba kwenye uwanja huo na kushinda mitano na kwenda sare mechi mbili.

Mabao ya Simba kwenye mchezo huo, yamefungwa na Medie Kagere kwenye dakika ya 30 ya mchezo mara baada ya kuuunganisha mpira uliopigwa na Bernard Morrison.

Dakika sita baadae, Dodoma Jiji walifanikiwa kuchomoa bao hilo kupitia kwa Clephace Mkandala akiunganisha mpira wa kona na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefungana ba0 1-1.

Kipindi cha pili, kilianza kwa kocha wa Simba, Didie Gomes kufanya mabadiliko mara baada ya kumtoa Luis Miquson na nafasi yake kuchukuliwa na Perfect Chikwende ambaye alikwenda kutengeneza bao la pili na la ushindi lililofungwa na Bernard Morrison kwenye dakika ya 67 ya mchezo, kwa shuti kali.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 38 ikiwa imecheza michezo 16, kwenye nafasi ya pili nyuma ya Yanga mwenye pointi 44 mara baada ya kucheza michezo 18.

Michezo miwili ya Simba iliyosalia ni Azam watakaocheza Jumapili tarehe 7 Februari 2021, saa 1:00 usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa na Namungo FC.

Ikiwa Simba itashinda mechi zote hizo mbili, itafikisha pointi 44 na kuwafanya kuongoza ligi kwa uwiano wa magoli.

Katika mchezo mwingine uliochezwa wa kiporo, KMC imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Namungo, mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dodoma.

Ushindi huo, umewafanya KMC FC kufikisha pointi 25, michezo 18 ikiwa nafasi ya sita huku Namungo ikisalia nafasi ya 15 ikiwa na pointi 18, baada ya kucheza michezo 15.

error: Content is protected !!