May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Simba yaipiga Coastal 7-0, Azam yapigwa kimoja

Spread the love

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Simba imetoa kipigo cha ‘mbwa koko’ cha 7-0 dhidi ya Coastal Union. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea)

Ushindi huo, umewafanya wekendu hao wa msimbazi ya jijini Dar es Salaam kufikisha pointi 23 ikisalia nafasi ya tatu ya msimamo wa VPL unaaongozwa na Azam FC ikiwa na pointi 25 baada ya kupigwa 1-0 na KMC.

Simba ikiwa mgeni wa Coastal Union Uwanja wa Sheikh Amri jijini Arusha leo Jumamosi tarehe 21 Novemba 2020, ilijiandikia magoli hayo kupitia kwa mshambuliaji wake, John Bocco aliyefunga matatu ‘hat trick’ dakika ya 24, 28 na 36.

Hat trick hiyo ilikuwa ya pili kufungwa VPL 2020/21 baada ya ile ya Adam Adam wa JKT Tanzania aliyoifunga dhidi ya Mwandui FC tarehe 25 Oktoba 2020.

Mlango wa magoli, ulianza kufunguliwa na Hassan Dilunga dakika ya 06 akitumia vizuri pasi aliyopewa na Bocco.

Dakika mbili za nyongeza za kipindi cha kwanza kabla hazijamalizika, Bernard Morrison aliifungia Simba goli latano na kuwafanya kwenda mapumziko ikiwa mbele ya magoli 5-0.

Dakika 45 za kipindi cha pili kilipoanza, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alifanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Bocco aliyefikisha magoli saba ya VPL na kumwingiza, Ibrahim Ajibu.

Coastal walianza kipindi cha pili kwa kushambulia na kucheza kandanda safi takribani takika tano kisha Simba ikarejea kwenye umiliki wa mpira.

Dakika ya 60, Clatous Chama aliiandikia Simba goli la sita baada ya kuwazidi mbio walinzi wa wagosi wa kaya.

Dakika ya 85, Chama tena alifunga idadi ya magoli kwa kufunga goli la saba kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Hadi dakika 90 zinamalizika, Simba imeondoka kifua mbele kwa ushindi huo wa magoli 7-0.

Katika mchezo mwingine uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam KMC imewafunga Azam 1-0.

Kipigo hicho kwa vinara wa VPL, Azam imewafanya kusalia na pointi zao 25 ikiwa inaongoza ligi hiyo huku KMC ikifikisha pointi 18.

Azam itaendelea kusalia kileleni kwa msimamo wa ligi hiyo, ikisubiri mchezo wa kesho Jumapili kati ya Yanga na Namungo FC utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Iwapo, Yanga yenye pointi 24 itaibuka na ushindi hiyo kesho dhidi ya Namungo yenye pointi 14 itafikisha pointi 27 na kuwafanya kuongoza ligi hiyo ikiwa imecheza michezo 11 sawa na Azam na Simba.

error: Content is protected !!