January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba yaikata ngebe Kmc, waishushia kichapo cha mabao manne

Spread the love

 

KLABU ya Simba imewakata ngebe Kmc ambao walitamba hapo awali kuondoka na ushindi kwenye mchezo huo, mara baada ya kuwabugiza mabao 4-1, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Mchezo huo ulipigwa hii leo tarehe 24 Desemba 2021, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, majira ya saa 10 jioni.

Kwenye mchezo huo ndani ya dakika 15 za kwanza Simba walifanikiwa kupata mabao mawili ya haraka kupitia mipira iliyokufa (Set Play).

Alikuwa nahodha kwenye mchezo wa leo Mohammed Hussen ndio aliyefungua pazia la mabao kwenye mchezo mara baada ya kuiandikia Simba bao la kwanza kwenye dakika ya 11.

Dakika mbili baadae beki kitasa Raia wa Kenya Josh Onyango aliandikia Simba bao la pili kwa njia ya mpira wa kona kwenye dakika ya 13.

Simba haikuishia hapo tu, kipindi cha pili kiliporejea Kibu Denis alionekana kuwa mwiba kwa watoto hao wa kiondoni mara baada ya kupachika mabao mawili kwenye dakika ya 46, 57’

Mara baada ya mchezo huo kocha mkuu wa kikosi cha Kmc, Habib Kondo yeye kwa upande wake alikili kuwa ndio mara ya kwanza toka kuanza kwa msimu mpya wa Ligi kikosi chake kupoteza kwenye mchezo mwepesi.

“Mchezo wa leo tumefungwa kirahisi sana, mabao yote tuliofungwa ni mapesi kwa sababu wachezaji wangu walikosa umakini kwenye eneo la uzuiaji, tumefungwa mechi rahisi kuliko zote” Alisema Kondo

Kwenye mchezo huo mabao matatu ya Simba yalipatikana kwa njia ya mipira iliyokufa ambapo bao la kwanza na bao la tatu yalipatikana kwa njia ya faulo huku bao la pili la Onyango likipatikana kwa njia ya kona.

Aidha kocha huyo aliendelea kusema kuwa bao lililomvutia kwenye mchezo ni bao la nne lililofungwa na Kibu Denis kwa shuti kali nje ya 18.

“Tumefungwa goli zuri moja alilofunga Kibu Denis kama mita 30 lakini mabao mengine yote yaliyobaki ni mipira iliyokufa kwa sababu wachezaji wangu walipoteza umakini.” Aliongezea kocha huyo

Kwa upande wa kocha wa Simba Thiery Hitimana yeye alisema kuwa wao walifanikiwa kupitia mipira iliyokufa ndio iliyowanufaisha.

“Sisi leo tulitumia nafasi tulizozipata hasa kwenye mipira iliyokufa ndio nafasi ambazo zimetunufaisha kuondoka na matokeo haya.” Alisema Hitimana

Kwa ushindi Simba bado inaendelea kusalia kwenye nafasi ya pili wakiwa na pointi 21, alama mbili nyuma ya Yanga wenye pointi 23 huku wote wakiwa wamecheza michezo tisa.

error: Content is protected !!