January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba vs Yanga, vita ya Tambwe na Okwi

Mashabikiwa timu za Simba na Yanga

Spread the love

MECHI ya watani wa jadi, Simba na Yanga itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, itakuwa na wachezaji 22, lakini vita itakuwa kati ya Amissi Tambwe na Emmanuel Okwi. Anaandika Erasto Stanslaus … (endelea).

Tambwe atavaa jezi ya Yanga akipambana na timu yake ya zamani ya Simba kwa mara ya kwanza, huku akiwa na hasira ya kutaka kuwaonesha kuwa walipoteza donge la dhahabu mkononi kwao na likaokotwa na wapinzani wao.

Okwi ambaye anaaminika kuwa ndiye alikuwa chachu ya ushindi mnono wa Simba wa mabao 5-0 katika mchezo uliochezwa Mei 6, 2012, leo ataingia uwanjani kuipa ushindi tena timu hiyo kwani tangu awape ushindi huo timu hiyo haijashinda mechi yoyote ya ligi dhidi ya Yanga.

Watani wa jadi Simba na Yanga wanakutana kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Machi 8, 2015 baada ya kutoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Tambwe ambaye alijiunga na Yanga mzunguko wa pili baada ya kusitishiwa mkataba na timu yake ya Simba aliyoitumikia kwa misimu miwili.

Mshambuliaji huyo wa Burundi aliyetwaa kiatu cha dhahabu msimu uliopita kwa kupachika mabao 19, ataingia uwanjani akiwa na hasira za kuachwa na Simba kwa madai kuwa ameshuka kiwango na badala yake kusajili washambuliaji wapya, Danny Sserunkuma na Simon Sserunkuma.

Tambwe ambaye ameshaifungia Yanga mabao manne tangu alipojiunga na timu hiyo, mawili katika ligi na moja katika michuano ya kimataifa, hivyo atakuwa na kibarua kingine cha kuwaonesha Simba kuwa bado yupo katika kiwango chake cha juu kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Mrundi huyo ambaye tangu ajiunge na Simba ameifunga Yanga mabao mawili pekee katika mchezo wa kwanza wa Nani Mtani Jembe uliomalizika kwa Simba kushinda 3-1, hivyo katika mechi ya mwishoni mwa wiki makali yake atahamishia kwa Yanga.

Okwi alirejea katika kikosi cha Simba mwanzoni mwa msimu huu baada ya kushindwana na Yanga, hivyo ataingia uwanjani kwa lengo la kuwasuta timu yake ya zamani kwa kuonesha uwezo na kuipa ushindi kama alivyofanya miaka miwili iliyopita.

Mshambuliaji huyo wa Uganda, tangu aipe Simba ushindi wa mabao 5-0 na kuondoka timu yake yaijawahi kuifunga Yanga katika mchezo wowote wa ligi hiyo baada ya kukutana nao mara sita na kutoka sare tano na kupoteza mmoja.

Okwi atakuwa na kibarua cha kuhakikisha anaipa ushindi timu yake hiyo katika mchezo wa mwishoni mwa wiki baada ya kushindwa katika mechi ya mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 18, 2014 na kumalizika kwa suluhu.

Pamoja na straika huyo wa Uganda kutokuwa katika kiwango chake kama kile alipovuna ushindi mnono lakini atataka kufuta mawazo hayo katika mchezo wa huo ili kuzima midomo ya mashabiki wa Yanga ambao wamekuwa wakimzomea kila anapokuwa uwanjani.

Baada ya Simba kushinda mabao 5-0 mwaka 2012, hawajavuna ushindi kwani walipokutana Oktoba 3, 2012 walitoka sare 1-1, Mei 18, 2013 walifungwa 2-0, Oktoba 20, 2013 sare ya 3-3, Aprili 19, 2014 sare ya 1-1 na Oktoba 18, 2014 ulimalizika kwa suluhu.

Simba walishindwa katika michezo yote miwili ya Nani Mtani Jembe, wa kwanza walishinda mabao 3-1 na ule wa pili waliibuka na ushindi wa 2-0.

Dakika 90 za mchezo wa Jumapili ndiyo utakaoweka historia mpya kwa timu hiyo pamoja na wachezaji hao ambao kila mmoja ana malengo yake katika mechi hiyo.

error: Content is protected !!