May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba: Tutawapiga Yanga 3, TFF leteni kombe uwanjani

Haji Manara

Spread the love

 

WAKATI joto la mtanange wa watani wa jadi Simba na Yanga za jijini Dar es Salaam, likizidi kupamba moto, Simba wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupeleka kombe la ubingwa uwanjani siku hiyo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Watani hao, watakutana katika nyasi za Uwanja wa Benjamin Mpaka, Dar es Salaam, Jumamosi hii tarehe 3 Julai 2021, kuanzia saa 11:00 jioni.

Mchezo huo wa watani, unawakutanisha wakati Simba bingwa mtetezi akihitaji pointi tatu muhimu ili kumwezesha kutetea ubingwa huo mara nne mfululizo huku Yanga ikihitaji kulinda heshima.

Simba ina nafasi kubwa ya kutetea ubingwa huo, kwani kati ya michezo mitano iliyobaki, inahitaji pointi nne tu.

Haji Manara

Kwa sasa Simba ina pointi 73 ikiwa imecheza michezo 29 huku Yanga ikiwa na pointi 67 baada ya kushika dimbani mara 31. Timu zinazoshiriki ligi hiyo ziko 18.

Leo Jumatano, tarehe 30 Juni 2021, Msemaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema, ikiwa mchezo huo utachezeshwa kwa haki, “goli chache zitakuwa tatu.”

“Niwaombe TFF kama itawapendeza, ituletee kombe letu uwanjani kama ambavyo tunaona huko kwingine wanafanya. Sasa kama tumeshinda ubingwa tunachelewa nini kukabidhiwa? Msiogope watakaolalamika ni kazi yao,” amesema Manara

Amewaomba waamuazi wa mchezo huo, kuzingatia sheria 17 za soka na kama mchezaji wa Simba akicheza rafu ndani ya eneo la penati basi penati itolewe na kusiwe na kigugumizi.

“Huu ni mchezo mkubwa, Onyago akicheza rafu ndani ya penati iweke penati, Wawa akicheza vibaya aonywe, kusiwe na ku-balance mchezo, marefa wakachezeshe kwa mujibu wa sheria 17 na ikifika saa 1 usiku, tunasherekea ubingwa wetu,” amesema

Msemaji huyo mwenye maneno mengi, amekumbushia ahadi iliyotolewa na viongozi wa Yanga kuwa msimu huu lazima ubingwa utakwenda mitaa ya Jangwani.

“Wenzetu waliapa msimu huu ubingwa wao, mpaka sasa wako kimyaaaa, hakuna anayehoji kiapo hicho kimeishia wapi. Na mechi yetu ikichezeshwa vizuri tutawapiga si chini ya goli tatu,” amesema Manara

“Sisi Simba ukiangalia kuanzia mwenyekiti wa bodi na bodi yenyewe na menejimenti chini ya CEO na sisi tunaoongoza idara tofauti tofauti, benchi la ufundi na wanachama, sisi dhamira yote ni moja tu, wanasimba ni furaha tu basi.”

“Hatuhitaji uongo uongo na uwekezaji wa Simba ni kuwapa watu furaha basi, ushindi tu, yaani Simba hawahitaji kingine, akitoka atambe mtaani, atambe mtandaoni, atambeee kokote,” amesema Manara

error: Content is protected !!