October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba SC. yang’ara, yawakung’uta 2:0 wahabeshi

Spread the love

KILELE cha Sherehe ya Siku ya Simba ‘Simba Day’ kimetamatika kwa kwa cheko la furaha baada ya kuibuka na ushindi wa bao 2:0 dhidi ya St. George kutoka nchini Ethiopia. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Mechi hiyo ya kirafiki iliyopigwa leo kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, imeshuhudiwa na maelfu ya mashabiki wa soka na klabu ya Simba kwa ujumla baada ya uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu 60,000 kujaa pomoni.

Iliwachukua dakika 18 Simba SC. kuandika bao la kwanza lililowekwa nyavuni na Kiungo mshambuliaji Kibu Denis aliyefumua shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa wageni hao ambao pia ni Mabingwa wa Ethiopia.

Hadi mapumziko Simba walikuwa kifua mbele kwa bao hilo moja, lakini katika kipindi cha pili ambacho kila timu ilifanya mabadiliko kwa kuingiza wachezaji zaidi ya watano, yalizidi kunogesha pilau la sherehe za Simba baada ya kupata bao la pili dakika  58.

Bao hilo la pili liliwekwa kimyani na mchezaji Nelson Okwa ambaye ni moja ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba katika msimu huu.

Bao hilo lilitokana na kazi safi iliyofanywa na Kiungo Mzambia, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ baada ya kunasa mpira uliopigwa na kugongwa mwamba kisha akambaambaa nao katika upande wa kulia na kuwalambisha mchanga mabeki wawili pamoja na kipa wa Wahabeshi hao ndani ya eneo la 18 na kutoa pasi mchongoma kwa Okwa aliyesukumia nyavuni bao la pili.

Kilele cha sherehe hizo kilipambwa na matukio mbalimbali ikiwamo, gwaride la halaiki, brasi bendi huku wasanii mbalimbali kama vile Zuchu na Tundaman wakiwapa raha mashabiki waliofurika katika uwanja huo.

error: Content is protected !!