January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simba Queen waichabanga Yanga Princess 4-1

Spread the love

 

DABI ya watani wa jadi kwa upande wa akina dada, Simba Queens na Yanga Princess imemaliza kwa wekundu hao wa Msimbazi kuwaadabisha akina dada wa Jangwani kwa bao 4 -1. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika mchezo huo ambao Yanga Princess walikuwa wakiwakaribisha Simba Queens, umepigwa katika dimba la Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

Ni sawa na kusema ‘Wananchi’ wameingia kwenye msitu mkali wakakutana na mnyama mkali Simba kilichobaki ni historia tu kwani ushindi huo umeendeleza rekodi ya ubabe wa Simba Queens mbele ya Yanga Princess.

Simba Queens wametoa vipigo kwenye msimu wao wa nne mfululizo na kuweka rekodi ya kushinda mechi sita kati ya saba ilizowahi kukutana na Yanga kwenye ligi.

Takwimu zinabainisha kuwa msimu wa 2018/19, Simba Queens ilishinda mabao 7-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kisha mabao 5-1 kwenye mzunguko wapili na msimu wa 2019/20 waliendeleza ubabe kwa kushinda mabao 3-1 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kabla ya mzunguko wapili kushinda mabao 5-1.

Msimu uliopita mchezo wa mzunguko wa kwanza Yanga iliambulia sare ya bila kufungana kule Mo Bunju Arena kabla ya kufungwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa mzunguko wapili.

Aidha, ushinidi wa leo umeifanya Simba kurudi kileleni kwenye msimamo wa ligi na kuishusha Fountain Gate ambayo ilikuwa inaongoza kwa alama tisa wakati Simba baada ya kushinda imekusanya alama 11.

Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Oppah Clement aliyefunga mawili pamoja na Asha Djafar ambaye pia alifunga mawili huku bao pekee Yanga likufungwa na Aisha Masaka kwa mkwaju wa penalti.

error: Content is protected !!