June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simanjiro wachangia maji na wanyama

Mifugo ya Ng'ombe

Spread the love

WAFUGAJI kutoka Kata za Narakawo na Lobosiret zilizopo wilayani Simanjiro, wamelalamikia tatizo la uhaba wa maji hivyo kulazimika kuchangia maji na mifugo katika Bwawa la Narakawo. Anaandika Ferdinand Shayo … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo na wananchi katika harambee ya uchangiaji ujenzi wa miundombinu ya maji iliyofanyika kwenye kata hizo.

Wananchi hao wamesema kuwa, kwa kipindi kirefu wamekua wakishiriki kutumia maji hayo na wanyama kutokana na kukosa huduma ya maji safi na salama hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya kuhara pamoja na typhoid.

Mwanakijiji Maria Edward amesema kuwa, wamekua wakipata shida ya maji na kulazimika kutumia maji ya bwawani ambayo hushirikiana na mifugo hivyo kupata magonjwa mara kwa mara.

“Maji tunayoyatumia yanatumika pia na mifugo na Bwawa tunalolitegemea tayari limebomoka jambo linalotupa wasiwasi wa upatikanaji wa maji, ujenzi wa visima na matanki ya kuhifadhia maji utasaidia kuondoa adha tunayoipata,” amesema.

Akizungumza katika harambee hiyo, mgeni rasmi Lenganas Mdele ambaye ni Mfanyabiashara amesema, wanakijiji hao hutembea umbali mrefu kilomita 30 wakitafuta maji na kutumia saa tisa kwa siku hivyo kushindwa kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi hali inayoathiri maendeleo ya jamii hususani kinamama wa kiwamasai.

“Tumeona haja ya kuunganisha nguvu kama wananchi kwa kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa matanki ya kuhifadhia maji yatakayowasaidia wananchi na kutatua kero ya hii inayowakabili kwa muda mrefu, katika harambee hii tumepata Sh.  Milioni 54 na ujenzi utaanza  mapema wiki hii,” amesema Lenganas. 

Mzee wa Kimila wa jamii ya Wamasai, Ezekiel Lesenga ameiomba serikali ijitokeze kuwaunga mkono katika juhudi zao kwani watu wa vijijini wamekua wakisahaulika katika masuala mbalimbali hususan huduma za kijamii kama vile maji, hospitali na shule.

error: Content is protected !!