May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Silinde amsimamisha mkuu wa shule, Takukuru yapewa kazi

Naibu Waziri Ofisi ya Rais- Tamisemi, David Silinde

Spread the love

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais- Tamisemi, David Silinde amemsimamisha kazi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Korona Jiji la Arusha,  Kashinde Mandari kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa mabweni mawili pamoja na bwalo la chakula na matumizi mabaya fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Amechukua maamuzi hayo baada ya kufanya ukaguzi katika shule na kujionea ujenzi ukiwa umesimama bila kuendelea huku fedha zote Sh.160 milion za bweni zikiwa zimemalizika hatua ya upauji.

Hali hiyo ni tofauti na halmashauri zingine za Monduli, Longido na Arumeru ambao wamemaliza kwa fedha hizo hizo walizopelekewa na serikali katika miradi ya lipa kwa matokeo (EP4R).

Katika hatua nyingine, Silinde ameagiza afisa elimu sekondari na mhandisi wa halmashauri kuandika barua ya kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kusimamia miradi hiyo na kutoa ushauri ambao umempotosha mwalimu huyo kutobana matumizi wakati wa ununuzi wa bei za vifaa vya ujenzi.

“Mimi nimekwenda katika halmshauri ya Longido nimekuta wamemaliza mabweni manne kwa gharama ya Sh.320 milioni ambalo kila bweni moja ni Sh.80 milion na yamekamilika kila kitu mpaka maji yanatoka.”

“Kule ni mbali tofauti na hapa jiji ambapo vitu ni bei rahisi sana lakini cha ajabu hapa mmenunua vitu gharama ya juu zaidi bila kubana matumizi kwa kuagiza kwa bei ya jumla kutoka kiwandani kama alivyofanya Longido na halmashauri zingine, angalia tu hata ujenzi wenyewe unatia mashaka sana hapa, nataka uchunguzi kujua thamani halisi ya fedha iliyotumika hapa,” amesema Silinde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi amesema wamepokea maelekezo ya Silinde na ameshaagiza ofisi ya Takukuru kuanza mara moja uchunguzi wa gharama zilizotumika shuleni hapo kwani hata yeye hakubaliani na gharama hizo na kusema mabweni hayo yatakamilishwa na mkurugenzi wa jiji kwa fedha za mapato ya ndani.

Katika kujitetea kwa naibu waziri, mkuu wa shule ya Korona, Kashinde Mandari na afisa elimu sekondari jiji la Arusha wamesema baadhi ya vifaa walikuta bei kubwa tofauti na ile iliyokuwa katika BOQ lakini zaidi walikuwa wanafuata ushauri wa mhandisi wa halmashauri ambaye muongozo ulipofika ulifikia kwake na yeye ndiye aliyewapotosha katika gharama za ununuzi wa vifaa vya ujenzi.

error: Content is protected !!