January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siku ya wanawake na mafanikio ya Beijing

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe

Spread the love

MACHI 8 kila mwaka, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), zinaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Uwekezaji Wanawake; Tekeleza Wakati ni sasa”.

Hivi karibuni Anna Maembe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii kutambua mchango wa wanawake katika kuleta maendeleo yao”.

“Pia ni sehemu ya kuelimisha wadau kuangalia upya wajibu wao wa kuwashirikisha, kuwaamini na kuwapa wanawake haki sawa katika nafasi za elimu, uchumi na uongozi ili waweze kuwa chachu katika maendeleo,” amesema Maembe.

Kwa upande wa Tanzania, maadhimisho haya yanatoa fursa kwa serikali, jamii na makundi mbalimbali ya wanaharakati yanayotetea haki za wanawake na watoto wa kike katika ngazi za taifa, mikoa, wilaya, kata, mitaa na vijiji kupima mafanikio yaliyopatikana katika kuendeleza wanawake.

Aidha siku hii inachukuliwa kama fursa pia ya kubainisha changamoto zinazojitokeza katika kuwawezesha wanawake na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa upande wa Tanzania, maadhimisho ya mwaka huu yanaambatana na kuwepo kwa matukio muhimu ambayo ni fursa katika kuhusisha masuala ya haki za wanawake na usawa wa jinsia.

Matukio haya yanajumuisha: Tathmini ya mafanikio ya utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing baada ya miaka 20 tangu kuidhinishwa kwake (1995-2015); tathmini ya Malengo ya Millenia (2005-2015).

Aidha, matukio mengine ni uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na mwelekeo wa Agenda 2063 kuhusu kuwa na ‘Afrika Tunayoihitaji’ ifikapo mwaka 2063.

Mbali na fursa hizo, bado wanawake wameendelea kukosa fursa mbalimbali katika nyanja zote kutokana na sababu za mfumo dume, mila potofu, sheria kandamizi na mfumo wa uliberali.

Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 imeruhusu mtoto wa kike mwenye umri chini ya miaka 18 kuolewa kwa idhini ya wazazi wake au mahakama.

Sheria hii imechangia ndoa za utotoni, mimba za utotoni, vifo vinavyotokana na uzazi, ukatili wa kijinsia na watoto walio katika ndoa kukosa maamuzi kuhusu maisha yao. Hivyo sheria hiyo inaathiri maisha ya mwanamke.

Takwimu zilizotolewa mwaka 2013 na Shirika la Umoja wa Mataifa, linalohusika na idadi ya watu (UNFPA), limeitaja Tanzania kama moja ya nchini ambazo zinakabiliwa na uongezeko kubwa la mimba za utotoni.

Mathalani kati ya mimba milioni moja zinazotugwa Tanzania, asilimia 23 ya mimba hizo zinawahusu wasichana walio chini ya umri wa miaka 19.

Baada ya kuanzishwa kwa mpango wa kurekebisha uchumi (SAP) mwanzoni mwa miaka ya 1980, kitaifa ulifungua milango ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma uliongozana na kuibuka kwa sekta binafsi huku serikali ikijitoa katika kutoa huduma za kijamii kwa asilimia 100 kama ilivyokuwa awali hasa elimu, afya na maji.

SAP ilikuwa na matokeo chanya na hasi. Lakini kwa kiasi kikubwa SAP imechangia kuongeza matatizo katika jamii. Wataalamu mbalimbali wanazikosoa sera za SAP hasa kwa kubana nafasi za wanawake hasa walio pembezoni.

Msukosuko wa mfumo wa kibepari unaoendelea katika mataifa mbalimbali, kwa kiasi kikubwa ameathiri nchi za bara la Afrika na Asia katika nyanja za kisiasa, kiuchmi na kijamii.

Aidha, msukosuko huo umepelekea Tanzania kurudi katika ukoloni mamboleo. Ukoloni ambao ulipigwa na mfumo wa kijamii kwa kuwa ulikuwa wa kinyonyaji.

Mataifa makubwa yaliyokumbatia mfumo huu na yenye mabavu yanahitaji rasilimali za Tanzania kwa nguvu na kwa msaada wa “mafisadi wa ndani” ambao wamepewa dhamana ya madaraka katika kuingia mikataba ya uwekezaji ambayo imefanywa kuwa ni “siri ya kikundi cha watu”.

Hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya Watanzania na kupelekea kuongezeka vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Hivyo, wakati tukitafakari kuhusu siku ya Wanawake Duniani ni muhimu uchambuzi wetu ukajikita katika masuala yaliyoibuliwa na wanawake wenyewe wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.

Masuala hayo yalijumuisha; haki za wanawake kubainishwa katika katiba mpya, sheria kandamizi zibatilishwe, utu wa mwanamke ulindwe, utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake na haki sawa katika nafasi za uongozi.

Masuala mengine ni; haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na kumiliki rasilimali ya nchi, haki ya uzazi salama, haki ya kufikia na kufaidi huduma za msingi, haki za wanawake wenye ulemavu, haki za watoto wa kike na kuwepo kwa Tume ya Haki za Wanawake na Mahakama ya Kifamilia.

error: Content is protected !!