August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siku 30 za ‘fungulia mbwa’ Ukawa Vs CCM

Dk. John Pombe Magufuli, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) (Picha kubwa) na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe

Spread the love

VYAMA vya siasa nchini kwa mara ya kwanza tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, vitaruhusiwa kufanya kampeni za majukwaani, anaandika Hamisi Mguta.

Vitatumia siku 30 kunyukana kwenye uchaguzi mdogo wa marudio utakaofanyika Tanzania Bara na visiwani na kisha kurudi kifungoni.

Hatua hiyo inafuatiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwaandikia barua ya kuviarifu vyama hivyo kufanya maandalizi ya kuingia kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika tarehe 22 Januari mwakani.

Uchaguzi huo utahusu ubunge katika Jimbo la Dimani, Zanzibar baada ya aliyekuwa mbunge wake, Hafidh Ali Tahir kufariki dunia alfajiri ya tarehe 11 Novemba mwaka huu.

Pia uchaguzi utafanyika kwenye kata 22 za Tanzania Bara ambapo kampeni zake zitachukua siku 30. Zitaanza tarehe 23 Desemba mwaka huu na kukoma tarehe 22 Januari, 2017.

Kwenye uchaguzi huo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine ikiwemo ACT Wazalendo vinatarajiwa kuanza kuwasha moto baada ya kutoka kifungoni mwa muda.

Ni wakati ambao vyama vya siasa vitakuwa huru kueleza wananchi mwelekeo wa nchi hadharani ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya mafanikio na mporomoko ya mwaka mmoja wa Serikali ya Rais Magufuli.

Mtifuano kwenye uchaguzi huo mbali na Zanzibar, mikoa mingine itakayohusishwa ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Arusha, Katavi, Mara, Sinyanga, Singida, Mwanza, Kilimanjaro, Pwani pia Kagera.

Ikumbukwe kuwa, kampeni hizo zitafanyika ikiwa ni zaidi ya miezi minne baada agizo la Rais Magufuli kuzuia mikutano ya kisiasa nchini mpaka 2020.

Rais Magufuli alieleza msimamo wake wa kutaka harakati za wazi za kisiasa kufanyika wakati wa uchaguzi mwaka 2020 na kwamba, wakati huu wa sasa ni wa kufanya kazi.

Msimamo huo ulipingwa na kada mbalimbali nchini kwa madai ya kuingilia uhuru wa wananchi pia kikatiba katika kuendeleza shughuli za kisiasa nchini.

Msimamo huo pia ulikwenda sambamba na kukamatwa kwa wanasiasa hususani wapinzani akiwemo Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar.

Pia Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema na  Edward Lowassa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema pia mgombea urasi wa chama hicho aliyeungwa mkono na Ukawa walikamatwa na kuhojiwa kwa madai ya kukiuka agizo hilo.

Msimamo wa Jeshi la Pilisi ulikwenda mbali zaidi na hata kupiga mikutano ya ndani ya vyama hivyo kwa madai ya kutumika kufanya uchochezi ili wananchi wasitii sheria za nchi. Baadaye waliruhusu.

error: Content is protected !!