July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siku 12 chungu kwa Halima Mdee, wenzake Chadema

Halima Mdee

Spread the love

 

HALIMA Mdee na wenzake 18, wamebakisha siku 12 kujua hatma yao juu ya uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ), kuwafukuzwa kwa tuhuma za usaliti. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Hatma yao itajulikana tarehe 31 Julai 2021, baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Chadema, kujadili na kuzitolea uamuzi rufaa zao, walizowasilisha kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu, tarehe 19 Julai 2021, jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amesema mkutano wa baraza hilo utafanyika tarehe 31 Julai mwaka huu, jijini Mbeya.

Mbowe amesema, baraza hilo litafanyika baada ya Chadema kumaliza kongamano lake la kudai katiba mpya, jijini Mwanza. Kongamano hilo litafanyika Jumatano, tarehe 21 Julai mwaka huu.

“Tukimaliza kongamano, tunaenda kufanya baraza kuu Mbeya tarehe 31 Julai 2021,” amesema Mbowe.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Katika mkutano huo, miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa na kutolewa maamuzi, ni rufaa ya Mdee na wenzake 18.

Mkutano wa baraza hilo ulikuwa unasubiriwa kwa hamu na baadhi ya watu hasa wafuasi na wanachama wa Chadema, ili kujua hatma za wanasiasa hao wanaokabiliwa na tuhuma za usaliti.

Baraza hilo limeitishwa siku kadhaa, tangu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuiandikia barua Chadema, akiitaka ijieleze kuhusiana na sakata hilo. Msajili huyo alikiandikia barua chama hicho tarehe 6 Julai 2021.

Mdee na wenzake walifukuzwa Chadema, siku mbili baada ya kuapishwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwa wabunge viti maalumu, tarehe 24 Novemba 2021.

Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na wenzake, walifukuzwa Chadema tarehe 27 Novemba 2021.

Kwa kosa la usaliti kufuatia hatua yao ya kuapishwa kuwa wabunge viti maalumu, kinyume na msimamo wa chama hicho wa kutopeleka wawakilishi bungeni, kikipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuuwa 2020.

Mbali na Mdee, wengine waliokata rufaa kupinga kutimuliwa Chadema ni, waliokuwa viongozi wa Bawacha, Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti). Grace Tendega (Katibu Mkuu). Jesca Kishoa (Naibu Katibu Mkuu) na Agnesta Lambart (Katibu Mwenezi).

Wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mtwara, Tunza Malapo.

Pamoja na Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropita Theonest na Conchesta Lwamlaza.

error: Content is protected !!