May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siku 100 za Rais Samia: Machozi, kicheko CCM

Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa CCM akizungumza na wajumbe wa chama hicho

Spread the love

 

KATIKA siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wapo wanachama wa chama hicho waliomwaga machozi kimya kimya na wapo walioangua kicheko cha furaha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kilio ama kicheko hutegemea na namna mabadiliko ndani ya chama hicho yalivyotafsirika na wahusika, kwa maana wapo waliopoteza nafasi zao na wengine kutwaa nafasi mpya ndani ya siku hizo.

Rais Samia aliingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Hayati John Pombe Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi mwaka huu, kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya moyo.

Rais Samia alitwaa uenyekiti wa CCM tarehe 30 Aprili 2021 baada ya kupigiwa kura na kupata za ndio kwa asilimia 100 (kura 1862 za wajumbe wote wa mkutano huo).

Baada ya kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa CCM, tarehe 30 Aprili 2021, katika Mkutano Mkuu wa chama hicho, aliteua wajumbe wa Sekretarieti ya CCM, ambao walithibitishwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Taifa (NEC), katika Mkutano Mkuu uliofanyika jijini Dodoma.

Mkutano Mkuu wa CCM

Mwenyekiti huyo wa CCM, alimteua Daniel Chongolo, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akichukua nafasi ya Dk. Bashiru Ally. Kabla ya uteuzi huo, Chongolo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Rais Samia alimteua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara na kumn’goa Rodrick Mpogolo kwenye wadhifa huo.

Mpogolo ameteuliwa na Rais Samia kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.

Katika kuendelea kupanga safu ndani ya CCM, Samia alizika jina la Humphrey Polepole ambaye ndiye alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wa mwisho kabla ya uteuzi mpya.

Nafasi hiyo, alikabidhiwa Shaka Hamdu Shaka ambaye sasa ni bosi wa Polepole.

Katibu wa Itikadi na uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka

Kabla ya Shaka kuteuliwa kwenye nafasi hiyo, nafasi hiyo ilikuwa wazi tangu Novemba 2020, baada ya Hayati Magufuli kumteua Polepole kuwa mbunge.

Mwenyekiti huyo wa CCM alimteua Maurdin Kastiko, kuwa Katibu wa NEC Oganaizasheni, akichukua nafasi ya Pereira Silima.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya CCM ambao Rais Samia hakuwagusa, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Sadala Mabodi ambaye alimuacha kuendelea na wadhifa huo.

Wengine ni Katibu wa Uchumi na Fedha CCM, Frank George Hawasi; Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM, Ngebela Lubinga.

Kishindo hicho cha Samia ndani ya CCM kiligusa pia uongozi wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), baada ya kumteua aliyekuwa mwenyekiti wake, Kherry James kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Kheri James, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, akiapa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla

Tarehe 19 Juni 2021, Samia aliteua wakuu wa wilaya akiwemo Kherry kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo. Hatua hiyo imesababisha nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM kuwa wazi.

Wakati nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM ikiachwa wazi, ya Makamu Mwenyekiti wa umoja huo pia iko wazi, baada ya aliyekuwa anashikilia wadhifa huo, Tabia Mwita kuteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kuwa Waziri wa Vijana.

Mabadiliko hayo pia yaligusa nafasi ya Katibu Mkuu UVCCM, ambapo Kamati Kuu ya CCM ilimteua Kenani Kihongosi kushika nafasi hiyo, akichukua mikoba ya Raymond Mangwala, aliyeteuliwa na Rais Samia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro.

Kwa mujibu wa Shaka, uchaguzi wa kujaza nafasi hizo, utafanyika baadaye.

error: Content is protected !!