Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Siku 100 Madarakani: Rais Samia hajagusa ‘mtima’
Habari za Siasa

Siku 100 Madarakani: Rais Samia hajagusa ‘mtima’

Spread the love

 

KATIBA na baadhi ya sheria kandamizi, zimetajwa kukwamisha kiu ya haki katika uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Hayo yamelezwa na baadhi ya wanasiasa pia wanaharakati wakati wakizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu siku 100 za Rais Samia madarakani.

Rais Samia anafikisha siku 100 akiwa madarakani, Jumapili tarehe 27 Juni 2021, baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, tarehe 19 Machi mwaka huu, akichukua mikoba ya Hayati John Magufuli, aliyefariki dunia akiwa madarakani.

Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi (CUF), Mhandisi Mohammed Ngulangwa, amesema katika siku 100 za Rais Samia madarakani, wananchi walitarajia kusikia kauli yake kuhusu upatikanaji katiba mpya.

“Kauli rasmi ya Rais Samia juu ya kilio cha wananchi wengi kuhusu katiba na tume ya uchaguzi haijasikika, badala yake wanasikika wasaidizi wake.  Hii inapelekea ionekane CCM ni ileile, sababu tatizo la Watanzania  ni katiba mpya,” amesema Ngulangwa na kuongeza:

“Na si hitajio la wapinzani, ikumbukwe mchakato wa kuipata katiba mpya ilitokana na maamuzi ya Serikali  ya CCM. Kukaa kimya kwa rais ndani ya siku 100,  bila kuzungumzia chochote kuhusu katiba mpya, inatia wasiwasi.”

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amesema katiba ya sasa inatoa  mamlaka makubwa, kwa viongozi wa ngazi za juu badala ya wananchi.

“Kwa ufupi anajaribu kupanga mambo yake lakini hajagusa wananchi.  Ili uwaguse wananchi inabidi abadilishe katiba. Katiba yake iko hovyo, imegusa watu wa juu tu, huku chini na kuendelea hakuna kitu ilichogusa,” amesema Rungwe.

Rungwe amesema, katiba iliyopo haikidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

“Katiba hii haijagusa wananchi kwa maana ya utawala, utawala ni wa chama kimoja ndiyo katiba hii ipo.  Haikugusa vyama vingi.  Si unajua rais anachagua mwenyekiti na mkurugenzi wa tume za uchaguzi,” amesema Rungwe na kuongeza:

“Mkurugenzi wa wilaya, wakuu wa wilaya na mikoa wote anachagua yeye na hawana kauli kwake. Wateule hao wana kauli  kwenye mashina ya mwisho.”

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi na Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, amesema baadhi ya mapungufu yaliyokuwepo katika Katiba, yanatia doa uongozi wa Rais Samia.

“Changamoto kubwa kwake bado hatujaisikia sauti yake akisema chochote kuhusu katiba mpya, kitu ambacho ilikuwa kilio chetu. Hiyo ni doa na dosari kubwa ambayo asipofanyia kazi yale yote mazuri anayofanya yataendelea kubakia changamoto,” amesema Olengurumwa na kuongeza:

“Mama Samia ajenge mifumo, anaonekana ana nia nzuri lakini ajenge mifumo ambayo yale yote anayofanya yalindwe na mfumo. Asilinde anayofanya sababu anaweza kutoka madarakani, yakapotea.”

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Fatma Karume, amesema  Rais Samia ameonesha dalili ya kufuata misingi ya utawala bora na sheria , lakini anakwamisha na mapungufu yaliyomo kwenye katiba na sheria.

“Ili aongoze vizuri kuna namna nyingi za kufanya,  lazima abadilishe katiba na sheria zilizopo, bila kubadilisha mfumo wa sheria, mfumo wa mahakama.  Hawezi kurejesha  imani kwa wananchi na wawekezaji,” amesema Fatma.

Fatma amesema “inabidi atazame suala la katiba mpya,  maana miaka mitano iliyopita imeonesha katiba hii ina udhaifu  mwingi sana, na inaoensha mtu mmoja anaweza kuja kuwa rais akabadilisha kila kitu, anauwa mifumo, anaua taasisi akawa yeye mungu mtu, .”

Mwanaharakati huyo amesema, ili nchi irudi katika utawala wa sheria, inatakiwa Katiba mpya.

 “Lazima abadilishe katiba ili kurudi kwenye utawala wa sheria, lazima hili jambo la katiba alifanyie kazi hawezi kuepukana nalo. Sababu hatuwezi kurudi katika utawala wa sheria kwa msingi huu,” amesema Fatma

Rais Samia ameingia madarakani baada ya Magufuli kufariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya moyo.

Rais Magufuli aliyeiongoza Tanzania kwa miaka mitano na miezi mitano mfululizo (Novemba 2015 hadi Machi 2021), mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!