July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Siku 10 operesheni kusaka wahamiaji haramu Loliondo

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Tanzania, Dk. Anna Makakala

Spread the love

 

KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji nchini Tanzania, Dk. Anna Makakala, ametangaza kuanza kwa operesheni maalum ya siku 10 kusaka wahamiaji haramu katika eneo la Loliondo Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Kamishna Jenerali Makakala amebainisha hayo leo Jumatano tarehe 22, Juni, 2022 alipotembelea tarafa ya Loliondo, na kusema kuwa zoezi hilo litaenda sawia na zoezi linaloendelea la uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo.

Dk. Makakala amesisitiza kufuatwa kwa sheria za nchi pale wageni wanapotaka kuingia au kutoka nchini, na kwamba Uhamiaji imejipanga vema kusimamia eneo hilo katika mipaka yote nchini.

“Nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na maeneo mazuri ambayo yanavutia wahamiaji haramu kufika nchini kwa sababu tofauti, hatutakubali hilo litokee wakati wowote ule,” amesema Makakala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala amemfahamisha Dk.Makakala kuwa wilaya yake inaendelea vema na utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo.

Pia amesema atatoa ushirikiano katika zoezi la kusaka wahamiaji haramu ili wale wote watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.

error: Content is protected !!