June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shule zasotea ruzuku

Mkurugenzi wa Haki Elimu Elizabeth Misokia

Spread the love

UFUATILIAJI wa Shirika la Hakielimu, umeaonesha kuwa kwa robo tatu za mwaka wa fedha, iliyoishia 31 Machi mwaka huu, Serikali imeweza kutoa asilimia tisa tu ya Sh. 10,000 kwa shule za msingi na asilimia 22 ya Sh. 25,000 ya ruzuku kwa sekondari kwa ajili ya kujiendesha. Anaandika Mwandishi Wetu…(endelea)

Kwa mujibu wa mipango ya maendeleo za shule ya msingi na sekondari (MMEM na MMES), shule zinapaswa kupata ruzuku kwa ajili ya kuziwezesha kujiendesha. 

Fedha hii inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa kununua vifaa, gharama za mitihani, ukarabati mdogo na kununua vitabu.

Shule za msingi zinapaswa kupata ruzuku ya Sh. 10,000 kwa mwanafunzi na shule za sekondari ni Sh. 25,000 kwa mwanafunzi.  Jumla ya fedha inayopaswa kupelekwa shuleni hutegemeana na idadi ya wanafunzi wa shule husika.

Kwa mujibu wa HakiElimu, imefanya ufuatiliaji wa hali ya ruzuku ya mwanafunzi katika wilaya 10 za Kilosa, Kilwa, Arusha vijijini, Iramba, Bariadi, Ukerewe, Serengeti, Kigoma Vijijini, Manispaa ya Tabora.

Jumla ya shule 40 za msingi na 40 za sekondari zilihusishwa. Takwimu zilikusanywa kati ya Machi 20 hadi 31mwaka huu.

Hakielimu wanasema “hii bado si dalili nzuri ya utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ambapo ilidhamiria kuhakikisha shule zinapata ruzuku ya asilimia 100 ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.”

Wanaongeza kuwa “ruzuku ya mwanafunzi ndio pesa zinazotegemewa na shule kwa ajili ya uendeshaji, hii inamaanisha kuwa shule nyingi sasa hivi zina uhaba wa fedha za uendeshaji na hivyo kuathiri upatikanaji wa elimu bora shuleni.

Mwaka wa fedha 2014/2015, ruzuku inaweza kupungua zaidi ya ile iliyotolewa 2013/2014. Uchambuzi wa takwimu za ruzuku ya mwanafunzi, umehusisha kiasi cha ruzuku kwa mwanafunzi kilichotolewa mwaka 2013/2014 na hali ya mwaka 2014/2015, inaonekana kuwa mbaya zaidi.

Shule zilizohusishwa katika ufuatiliaji huo zina changamoto ya ukosefu wa fedha na hali hii inaathiri shule kupata mahitaji ya msingi kama chaki, vifaa vya ofisi na kukabili gharama ndogo za uendeshaji.

Hakielimu wanashauri “Hivyo ikiwa imebaki miezi miwili kumaliza mwaka wa fedha 2014/2015, serikali ipeleke fedha za ruzuku kwa shule za msingi na sekondari. Kitengo cha Utekelezaji wa BNR cha ofisi ya Rais hakina budi kufanya mawasiliano na Wizara ya Fedha,Wizara ya Elimu na Twala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha fedha za ruzuku ya mwanafunzi zinapelekwa shuleni katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2015.”

error: Content is protected !!