October 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shule za serikali zawakera wabunge

Shule ya Msingi Juhudi iliyopo Wilaya ya Kigoma Vijijini mkoani Kigoma nchini Tanzania wakiwa darasani

Spread the love

MBUNGE wa Viti Maalum, Amina Abdallah Amour (CUF) ameitaka serikali kueleza ni lini itaboresha shule zake ili wazazi wasishawishike kuwapeleka watoto katika shule zilizopo nje ya nchi. Anaripoti Dany Tibason kutoka Dodoma … (endelea).

Alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza alipotaka kutaka kujua ni lini serikali itaboresha shule zake ili wazazi wengi wasiwapeleke watoto wao katika shule ambazo zipo nje ya nchi.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema) akiuliza swali la nyongeza, alitaka kujua kauli ya serikali kama ina mpango wa kupiga marufuku kuwapeleka watoto katika shule za kulala.

“Hivi karibuni nimemsikia Rais wa Rwanda akipiga marufuku kuwapeleka watoto chini ya miaka sita kuwapeleka katika shule za kulala. Je kauli ya serikali ni nini kwa wazazi ambao wanawapeleka watoto wao katika shule za kulala?

“Watoto wengi waliopo chini ya miaka 14 wanatakiwa kuwa karibu na wazazi wao ili kujifunza mambo mbalimbali lakini kwa sasa wazazi wengi wanapeleka watoto wao katika shule za kulala wakiwa na umri mdogo nini kauli ya serikali kwa jambo hilo?” alihoji Lyimo.

Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa Kimwanga (CUF) alitaka kujua ni sababu gani zimechangia kupungua kwa idadi kubwa idadi ya wanafunzi wanaokwenda kusoma Kenya na Uganda.

Akijibu maswali ya nyongeza, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango amesema, wazazi wengi waliokuwa wakipeleka watoto wao katika nchi hizo walikuwa na malengo ya watoto wao wapate elimu ya Kiingereza kwa kujua kusoma na kuandika.

Amesema, watoto waliokuwa wakipelekwa katika shule hizo siyo kweli kuwa walikuwa wakipata elimu nzuri bali wazazi waliamini kuwa watoto wao wataweza kuandika na kusoma vizuri Kiingereza.

Kuhusu watoto wadogo kupelekwa katika shule za kulala amesema kuwa, siyo jambo jema kumpeleka mtoto katika shule za kulala.

“Mtoto wa chini ya miaka 14 hastahili kupelekwa katika shule za kulala na mimi kama mzazi nashauri kuwa si vyema kumpeleka mtoto chini ya miaka 14 katika shule za kulala.

“Watoto hao wanahitaji kupata malezi ya wazazi na sipendi kuzungumzia mambo ya nchi ya watu wengine lakini ni bora wazazi wakatambua kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa wazazi kuwa na watoto wao karibu katika kipindi cha umri huo” amesema Kilango.

error: Content is protected !!