BENKI ya Exim imetoa Sh.10 milioni kwa taasisi ya Asma Mwinyi Foundation (AMF), kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa vifaa vya ujenzi na ukarabati vyoo vya shule ya awali, msingi na sekondari ya Kandwi, Unguja, visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu, amesema, wanatambua changamoto za elimu visiwani hivyo, “tumejitolea kuhudumia watu, biashara na jamii kwa ujumla.”
“Tunafurahi kuwa sehemu ya mkakati huu muhimu unaolenga kuinua mazingira ya elimu Zanzibar. Tunaona taasisi ya AMF kuwa mshirika sahihi katika kufanikisha dhamira hiyo,” amesema Kafu
Alisema, wana dhamira inayofanana kati ya benki hiyo na AMF ya kusaidia juhudi za kielimu na ustawi wa wanafunzi na shule kote nchini.
“Wanafunzi hutumia muda mwingi zaidi katika siku wakiwa shuleni hivyo ni muhimu zaidi tukiweka jitihada katika kuboresha mazingira ya vyoo vyao,” alisema.
Naye Asma, aliishukuru benki hiyo huku akibainisha kuwa, msaada huo utagusa maisha ya wanafunzi wengi kwa miaka mengi ijayo.
“Wadau wetu muhimu na washirika kama Benki ya Exim, ndio nguzo muhimu kwa mafanikio yetu. Tunashukuru kwa msaada huu ambao utasaidia katika kukarabati vyoo vya shule ya awali, msingi na sekondari ya Kandwi,” alisema
Wawakilishi wa shule hizo, Kheir Juma Pandu na Juma Haji Ame walisema, kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa vyoo hivyo kutasaidia kuhudumia wanafunzi zaidi 700 waliopo katika shule hiyo.
Leave a comment