August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shule binafsi zalia na serikali  

Wanafunzi

Spread the love

SERIKALI imeombwa kuwasaidia wamiliki wa shule binafsi mkoani Dodoma kupatiwa mikopo kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii ili shule zao ziweze kuchukua wanafunzi wengi, anaandika Mwandishi wetu.

Mbali na hilo, pia imeombwa kuwaingiza katika mgao wa kupata vitabu shule binafsi kama inavyofanya katika shule za serikali.

Maombi hayo yalitolewa jana na Mkurugenzi wa shule ya msingi ya El Shaddai iliyopo mjini hapa Juliana Assey katika katika mahafali ya nne ya darasa la saba ya shule hiyo.

Amesema wamiliki wa shule hizo wanatamani kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya elimu lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya uwezo mdogo kifedha.

Amesema kutokana na uwezo huo wanashindwa kufanya jambo lolote kwa haraka kama ujenzi wa majengo mengine ili kuendana na kasi ya serikali kuhamia Dodoma.

Mkurugenzi huyo amesema iwapo serikali itawasaidia waweze kukopeshwa fedha au kujengewa majengo na mifuko ya hifadhi za jamii wataweza kuendana na kasi hiyo.
“Serikali wakati mwingine imekuwa ikitumia mifuko ya hifadhi ya jamii kujenga taasisi zao

wenyewe,hivyo sisi kama wamiliki wa shule binafsi tungependa utaratibu huo utumike pia kwetu kwa kutujengea majengo tunayotaka na tutalipa kwa kuwa mabenki hawataki kutukopesha kwa kutumia dhamana ya shule,”alisema mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usajili wa shule, Khadija Mcheka ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wanapata elimu katika mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

“Sisi kama serikali tunahakikisha hakuna ubaguzi kwa uteuzi wa wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari bali tunachoangalia ni uwezo wa mwanafunzi kitaaluma,hivyo wahitimu muwe na amani na msiwe na mashaka,”alisema Mcheka.

Naye, Mwalimu mkuu wa shule hiyo Silas Ntiyamila aliwataka wahitimu hao kuwa wazalendo,kutunza mazingira na kujiepusha na mambo yasiyokuwa na maadili.

Awali, akisoma risala mmoja wa wahitimu hao, Aliyah Kamando amesema pamoja na changamoto zinazowakabili shuleni hapo ikiwemo ukosefu wa maktaba,nyumba za walimu na maabara ya kompyuta lakini wanaahidi kufanya vizuri kwenye mitihani yao kwa kuwa wasomi wa leo ndio viongozi wa kesho.

error: Content is protected !!