June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shivyawata wamvaa Ummy Mwalimu

Spread the love

SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) limeitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee kuwatambua watu wenye ulemavu kama kundi linalostahili kupata msamaha katika ulipiaji wa gharama za huduma za afya, anaandika Pendo Omary.

Hatua hii inakuja ikiwa ni siku nne tu tangu Ummy Mwalimu,  Waziri wa wizara hiyo kuyataja makundi matatu yanayostahili kupata msamaha wa gharama za matibabu kuwa ni; watoto, wazee na wanawake wajawazito pekee.

Ummy Nderiananga, Mwenyekiti wa Shivyawata amewambia wanahabari leo jijini Dar es Salaam kuwa taarifa ya waziri Ummy Mwalimu kutolitaja kundi la walemavu kama sehemu ya makundi yanayosahili msamaha wa gharama za matibabu imeibua mjadala wenye hisia tofauti hasa kwa watu wenye ulemavu.

“Shivyawata inamtaka Waziri Ummy Mwalimu kuhakikisha kwamba waraka wa afya wa mwaka 2012, unawafikia watoa huduma za afya wa serikali kwani watu wenye ulemavu tunakabiliana na changamoto ya kutakiwa kuonyesha utambulisho maalumu kutoka serikali za mitaa. Walemavu hatustahili kuhurumiwa bali kuzingatiwa kwa haki yetu ya msingi ya kupata huduma za afya bure kama makundi mengine,” amesema.

Nderiananga ameitaka Wizara ya Afya kufanya maboresho ya waraka wa afya wa mwaka 2012 ili huduma ya tiba bila malipo kwa walemavu isiishie kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati, bali pia katika hospitali za rufaa.

“Lakini pia Shivyawata tunaitaka Wizara ya Afya kutoa bima maalum za afya kwa watu wenye ulemavu ili kuepuka udhalilishaji na urasimu katika kupata huduma hizo katika vituo vya afya, zahanati na hospitali zote,” amesema Nderiananga.

error: Content is protected !!