January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shilingi ya Tanzani hoi, Mbatia aonya

Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, James Mbatia akizungumza na waandishi wa bahari leo jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) kuhusu kuporomoka kwa thamani ya Shilingi.

Spread the love

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imetakiwa kutoa fedha za kigeni kwenye mzunguko ikiwa ni hatua ya haraka ya kukabilina na kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Anaandika Pendo Omary …(endelea).

Mbali na hatua hiyo, pia BoT imetakiwa kutoa matumaini kwa Watanzania kuhusu hali ya uchumi nchini.

Kauli hiyo, imetolewa na James Mbatia – Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge.

Mbatia ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi na vile vile mbunge wa kuteuliwa, amesema “hatua hii itasaidia kuiokoa shilingi tofauti na hali ilivyo sasa.”

“Thamani ya shilingi ya Tanzania imekuwa ikiporomoka kwa kasi ya kutisha. Ndani ya mwezi mmoja tu, shilingi yetu imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 kutoka Sh. 1,650 kwa Dola moja ya Kimarekani hadi Sh. 2,010 (kwa takwimu za jana),” amesema Mbatia.

Amesema mporomoko huo ni tishio kwa uchumi wa nchi huku sayansi ya anuai ikionesha kwamba nguvu ya mporomoko wa kiasi hiki, unaweza kutikisa vibaya mfumo wa uchumi kama hatua za kifedha hazitachukuliwa haraka iwezekanavyo na taasisi husika.

Akizungumzia kuhusu mambo ya ndani ya nchi ambayo yamechangia kuporomoka kwa shilingi, Mbatia amesema “mambo hayo yapo makuu manne: bajeti ya Taifa inayotegemea wafadhili; mauzo kidogo kutoka ndani kwenda nje ya nchi; manunuzi makubwa kutoka nje kuja ndani ya nchi na siasa sizizokuwa na hofu ya Mungu hasa ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow.”

“Kwa kuwa bajeti ya taifa kwa zaidi ya asilimia 30 inategemea fedha za wafadhili wa miradi ya maendeleo, baada ya ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow, waligoma kutoa fedha. Hii imechangia mporomoko wa shilingi kutokea,” amesema Mbatia.

Aidha, Mbatia amesema uwezo wa Tanzania kuongeza mapato kutoka mauzo ya nje ni mkubwa. Sekta za uvuvi, utalii na usafiri wa anga zinaweza kutumika kwa haraka ili kuongeza fedha kutoka nje na kukabiliana na mporomoko wa shilingi.

Ameongeza kuwa “hivi sasa manunuzi yetu ya nje ni makubwa kulingana na mauzo yetu nje. Manunuzi hayo hutumia fedha za kigeni. Hii ina maana tunahitaji fedha nyingi zaidi za kigeni katika kubadilishana bidhaa na huduma kuliko shilingi. Mambo haya yanadhihilisha kwamba hatutambui au kuthamini utaifa wetu”.

Mbatia ameshauri kuwa ili kukabiliana na mporomoko wa shilingi lazima sheria za manunuzi ya bidhaa za nje zitiliwe mkazo.

error: Content is protected !!