December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shigongo ataka wasio waadilifu wachapwe viboko

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo

Spread the love

 

MBUNGE wa Buchosa, Eric Shigongo (CCM) amependekeza watumishi wa umma wasio waadilifu wachapwe viboko ili kukomesha ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na kuwalazimisha watumishi hao kuwa waadilifu. Anaripoti Gabriel Mushi, Dar es Salaam … (endelea).

Aidha, amesema kama Serikali haitotaka kuwachapa viboko basi itumie sheria tano zilizopitishwa na Bunge ambazo ni pamoja na Sheria ya Takukuru, sheria ya fedha, utakatishaji fedha, manunuzi na uhujumu uchumi kuwawajibisha watumishi hao wasio waadilifu.

Shigongo ametoa mapendekezo hayo leo bungeni jijini Dodoma tarehe 5 Novemba, 2022 wakati akichangia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa.

Amesema katika halmashauri yake ya Buchosa, ndani ya ripoti hiyo amebaini kuna ubadhirifu wa Sh milioni 94 jambo ambalo anaona aibu hasa ikizingatiwa waliokula fedha hizo bado wapo uraiani.

Amesema Tanzania inaumwa magonjwa mawili ambayo ni ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji.

Amesema licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kutumia muda was aa 263 angani kuelekea katika nchi mbalimbali kutafuta riziki kwa ajili ya Watanzania bado, taasisi za Serikali zinaumwa magonjwa hayo mawili.

“Ninavyozungumza unaweza kusema Tanzania ina mfumuko mkubwa wa bei lakini mfumuko wa bei Sudani ni asilimia 285, Kenya ni asilimia 6.7, Uganda ni asilimia saba na Tanzania ni asilimia 4.4. Tanzania ni nchi yenye mfumuko mdogo wa bei katika nchi za Afrika Mashariki,” amesema.

Amesema tangu awe mbunge ripoti ya CAG ikija bungeni inasema watu wameiba watu wameiba, lakini si kwamba hakuna watu wasio waadilifu.

Amesema kinachoshangaza watu wasio waadilifu serikali siku hizi ni mashujaa kwani wanastaafu wakiwa matajiri, ilihali wasio waadilifu wanastaafu wakiwa maskini na kuonekana wajinga.

Akinukuu kitabu cha Mwandishi maarufu Jack Welch chenye jina la ‘straight from the gut’, ambaye alipendekeza njia mbili za kuongoza watu ambazo kwanza ni kuwasihi ili waende na wewe au kuwalazimisha waende, Shigongo alichagua njia ya pili ya kuwalazimisha.

Amesema mbali na kupandikiza uadilifu kwenye mioyo ya watoto kwa kutumia mitaala au njia nyingine yoyote, kwa watu wazima walioshindikana amesema waarabu husema punda haendi bila bakora.

“Ingekuwa mamuzi yangu, ningependekeza tuwe na siku ya uchapaji viboko kitaifa, fimbo zitoke Mbeya wachapaji watoke Tarime, ukishabainika unaitwa unaenda mbele unachapwa,” amesema na kuongeza;

“Neno la Mungu kutoka katika kitabu cha Mathayo 12;25 linasema Taifa lolote linalopingana na lililogawanyika haidumu na nyumba yoyote inayopingana na iliyogawanyika hufa. Hivyo, tusimame pamoja kwenye suala hili kukomesha wezi kwenye Taifa letu inawezekana tutakumbukwa na watoto na wajukuu watasema Bunge la 12 Dk. Tulia Ackson lilibadilisha Taifa letu,” amesema.

error: Content is protected !!