April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shibuda atibua hali ya hewa mkutano wa Chadema, kisa Rais Magufuli

John Shibuda, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania

Spread the love

JOHN Shibuda, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, amechafua hali ya hewa katika Mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kumsifia Rais John Magufuli. Anaripoti Hamis Mguta …(endelea).

Shibuda ni mmoja ya wasasiasa walioalikwa katika mkutano Mkuu wa Chadema unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti huyo ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha ADA-TADEA, pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Maswa kwa tiketi ya Chadema, alipewa nafasi ya kuhutubia katika mkutano huo, lakini alivuruga hali ya hewa baada ya kudai kuwa haamini kama Rais Magufuli, atafuta mfumo wa vyama vingi.

Shibuda amesema kuwa Rais Magufuli hawezi kufuta mfumo huo kwa sababu imani yake ni kuheshimu, kusifu pamoja na kumuenzi muasisi wa taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema Mwalimu Nyerere alitoa nasaha na zikazaa mfumo wa vyama vingi kwa hiyo ukitaka kufuta mfumo wa vyama vingi maana yake unataka kumfuta Baba wa taifa.

https://youtu.be/EysUGUwIXrk

Aidha, ameeleza kuwa aliwahi kukutana na Rais Magufuli na kumuuliza kuhusu kuzuia mfumo wa vyama vingi na akamueleza kuwa; “Sizuii mfumo wa vyama vingi lakini naomba mfumo huo usiwe na lugha za kudhalilishana.”

Baada ya kuzungumza hayo wajumbe waliopo ndani ya ukumbi huo walianza kupiga kelele huku wakigonga meza wakimtaka Shibuda asitishe hotuba yake na kushuka jukwaani, ikiwa ni ishara ya kutokubaliana na alichokizungumza.

Hali hiyo ilichukua takriban dakika tano, huku Shibuda akiendelea kusubiri hali itulie ili aendelee na hotuba yake, lakini wajumbe nao waliendelea kupiga kelele, hivyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alilazimika kupanda jukwaani ili kuwatuliza.

“Nawaomba muache fujo. Mtu akizungumza hata kama ametukosea tumsikilize na ndiyo maana kauli mbiu yetu kuu katika mkutano huu ni ‘No Hate, No Fear,’ alisema Mbowe.

Wajumbe wa mkutano huo walimtii mwenyekiti wao na kumruhusu Shibuda kuendelea na hotuba yake lakini hakuzungumzia tena kilichowakera wanachama wa Chadema.

error: Content is protected !!