August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheria ya Ugaidi yawakera Waislam

Spread the love

SHERIA elekezi inayotumiwa katika kukabiliana na ugaidi nchini na dunia zima ina uonevu mkubwa kwa kuwa, wanaohusishwa nayo wengi wao si magaidi, anaandika Faki Sosi.

Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini amesema kuwa, sheria hiyo ni moja ya mbinu chafu za mataifa bepari katika kuwagawa watu na kupandikiza chuki.

Amesema hayo leo katika Viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam baada ya ibada ya Swala ya Idd ambayo imetekelezwa na Waislam wote ulimwenguni.

Amesema kuwa, takwimu za watu wanaouawa katika matukio mbalimbali inaonesha ni vijana wa kiislam.

Amesema, ukifuatilia mwendendo wa vijana hao unabaini kuwa ni miongoni mwa vijana wema katika jamii ambapo jeshi la polisi huwatuhumu kuwa majambazi.

Ponda ameonesha wasiwasi juu ya tukio lililofanyika Mwanza na Tanga kwamba, huenda limefanywa makusudi na watu ambao si waislam ili kuonekana kuwa waislam wabaya.

Amebainisha wasiwasi wake kati ya taarifa ya Jeshi la Polisi kuwa, watu hao waliuawa na watu waliovaa soksi usoni mwao na kwamba, waliitaja idadi ya wavamizi hao.

Hata hivyo amehoji, walizimaa taa na kutekeleza mauji hayo, Je polisi walipata wapi ushahidi wa kueleza kuwa walikuwa katika mazingira gani na idadi yao? “Ni uongo wa wazi.”amesema na kuongeza kuwa, kila siku polisi wanaendelea kutoa taarifa zenye utata kuhusu wahusika wa mauaji hayo.

Hata hivyo amedai kuwa, askari wanapokwenda kuchukua mafunzo ya kupambana na magaidi huambiwa kuwa gaidi ni mfuga ndevu.

“Ukitaka kuumua mbwa mpe jina baya” amesema Sheikh Ponda.

Amesema kuwa, nchi za Magharibi hulazimisha sheria hizo ambapo Tanzania ililetewa muswada huo ulopingwa na kila mtu wa dini zote pamoja na wabunge kwa kujua madhara yake kwamba watagawa watu.

“Lakini Marekani walilazimisha sheria na kuupitisha muswada ule mwaka 2002 na madhara yake yanajitokeza sasa” amesema.

Amesema kuwa, sheria hiyo inawaadhibu watu wasio kuwa na hatia ilimradi ni waislam na kwamba, yeye pia alisota jela kwa sheria hiyo yenye nia mbaya kwa taifa.

Dk. Abdallah Tego wa Chuo Kikuu cha kiislam Morogoro(MUM), amesema kuwa uislam ni dini yenye kusisitiza amani hata tafsiri ya dini hiyo ni amani na salam ya dini hiyo ni amani hivyo waislam wote ni watu wa kupenda amani ingawa kuna watu wanataka kuutia doa uislam.

Amesema kuwa, kitabu kitukufu cha quran kimeeleza kuwa mauji ni miongoni mwa madhambi ambayo Mungu hatoyasamehe.

Amesema kuwa mauaji ya hivi karibu katika mji mtukufu wa Madina na sehemu nyingine duniani huonesha jinsi gani watu wasiokuwa na nia nzuri na uislam wanavyochafua na kuwauwa waumini wa dini hiyo.

Mwisho amesisitiza vijana na wazee wa kiislam kuwasomesha vijana hao elimu ya dini na ya dunia.

error: Content is protected !!