August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheria usafirishaji Ziwa Victoria yaiva

Spread the love

KUANZA utekelezaji wa sheria ya usafirishaji Ziwa Victoria ya mwaka 2007 kwa Nchi za Afrika Mashariki, itasaidia kuleta mageuzi kwenye sekta ya usafiri majini na kuimarisha ulinzi na usalama wa vyombo vya majini, anaandika Moses Mseti.

Hayo yameelezwa leo na wadau pamoja na watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali jijini Mwanza, mbele ya John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, walipokutana kujadili utekelezaji wa sheria hiyo huku sheria hiyo ikitarajia kuongeza ufanisi na utendaji kazi katika Ziwa Victoria.

Mhandisi Gerson Fumbuka, mwakilishi kutoka Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ambaye ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa usafiri majini amesema, sheria hiyo inajikita katika kuboresha maeneo yenye vipaumbele yakiwamo vitendea kazi, ufanisi wa utoaji taarifa, kuongeza uokoaji na utafutaji watu waliozama.

“Hii itakwenda sambamba kwa kuongeza vitendea kazi kama taa (traffic lights) na maboya, ufanisi wa utoaji taarifa za hali ya hewa, kuongeza uokoaji na utafutaji wa watu hasa katika majanga.

“Pia hiyo itasaidia vyombo visichafue ziwa na kupunguza maafa kwa samaki, pamoja na kuhakikisha kina cha bandari kinaongezeka ili kuruhusu meli zote kufika kwa kuhakikisha tunapunguza mchanga unaosababisha meli zishindwe kuchukua abiria,” amesema.

Kapteni Mussa Mandia, Msajili wa Meli akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini amesema, kutokana na Tanzania kuendelea kutumia sheria ya usafirishaji wa meli za mizigo (Merchandise Shipping Act) kwa muda mrefu katika kuendesha vyombo vya usafiri majini, kuna haja ya kutumia kanuni na sheria za pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki.

“Tunategemea kuboresha ulinzi na usalama wa vyombo vya majini, na kwa kupitia sheria hii hali itakuwa bora zaidi kama tutaipa kipaumbele sheria hii na tuwe mfano wa kuigwa kwa wenzetu,” amesema Mandia.

Marry Onesmo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana akizungumza amesema, sheria hiyo imetengezwa kwa kutambua maendeleo ya sekta ya ziwa katika usafiri wa majini katika ukanda wa Ziwa Victoria kwa nchi husika.

“Ziwa Victoria limekuwa ni kitovu muhimu cha usafirishaji majini wa watu na mizigo kutokana na kuongezekana kwa shughuli za biashara, ongezeko la watu, na kukua kwa miji kandokando ya ziwa hili hasa Jiji la Mwanza” amesema.

Marry ameongeza kuwa, sheria itasaidia kunganisha usafiri wa reli na barabara kutoka sehemu ya ziwa kwenda ng’ambo nyingine, ikiwa ni uboreshaji wa shughuli za bandari, na kuongezeka kwa shughuli za uvuvi pamoja na utunzaji wa mazingira unaosababishwa na vyombo vya usafiri majini.

Bandari ya Mwanza ni moja kati ya bandari zenye usajili wa meli nyingi katika nchi zinazozunguka Ziwa Victoria na kupitia Sumatra bandari ya Mwanza imesajili meli 46 zinazotoa huduma za usafiri.

error: Content is protected !!