Tuesday , 30 May 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Sheria nyingine ‘katili’ yaja, ni ile ya Majengo, sasa hadi matembe kulipa kodi
Habari za SiasaTangulizi

Sheria nyingine ‘katili’ yaja, ni ile ya Majengo, sasa hadi matembe kulipa kodi

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi
Spread the love

SERIKALI ya Rais John Pombe Magufuli, sasa imeamua “kula matapishi yake.” Jumamosi wiki hii, inarudi tena bungeni kuwasilisha mabadiliko mengine kwenye Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma … (endelea).

Marekebisho ya sheria ya madini yanafanyika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu, tangu kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa marekebisho hayo.

Sheria mpya ya madini ijulikanayo kama The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2017, ilianza kutumika 7 Julai 2017. Sheria mpya ilifanyia marekebisho lukuki sheria ya madini ya mwaka 2010.

Kufuatia hatua hiyo ya serikali, mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri, ambao ulipangwa kumalizika Ijumaa wiki hii, sasa utamalizika Jumamosi ya tarehe 9 Februari 2019.

Mabadiliko katika sheria hii, yanakuja takribani wiki tatu tangu Rais Magufuli akutane na wadau wa madini wakiwamo wachimbaji wadogo.

Miongoni mwa marekebisho yaliyofanyika katika sheria ya madini ya mwaka 2010, Julai mwaka 2017, ni pamoja na kuanzishwa kwa Tume ya Madini (Mining Commision) na kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (Tanzania Mineral Audit Agency- TMAA).

Marekebisho mengine, ni kuongezeka kwa malipo ya mrabaha kutoka asilimia 4 kwa madini ya Metali (mfano dhahabu, shaba, fedha n.k) hadi asilimia Sita; ongezeko la malipo ya mrabaha kwa madini ya almasi na vito – Tanzanite, Ruby, Garnets na mengineo – ambayo ni kutoka asilimia tano hadi Sita.

Aidha, muswada ulieleza kuwa kupitia marekebisho ya sheria ya fedha na sheria ya kodi, kila mtu au kampuni anayetaka kusafirisha madini, sharti afanyiwe ukaguzi na kuthaminishwa na anapaswa kulipia binafsi ada ya ukaguzi huo (clearing fees).

Kwa mujibu wa sheria, ada ya ukaguzi ni asilimia moja ya thamani ya madini yanayosafirishwa.

Naye mchimbaji mdogo anayeuza madini kwa mtu wa kati, Broker au Dealer anatakiwa kukatwa asilimia 5 ya thamani ya madini kama kodi itakayokusanywa na mnunuzi na kupelekwa Mamlaka ya Mapato ya Taifa (TRA).

Katika hatua nyingine, mara baada ya sheria hiyo kuanza kutumika, serikali ilitangaza kusitisha utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji madini. Ilisema leseni mpya zitatolewa baada ya tume ya madini kupatikana na kuanza kazi.

Marekebisho ya sheria hiyo, yalipingwa vikali na wabunge wa upinzani kwa maelezo kuwa yanalenga kuvuruga sekta ya madini. Hawakusikilizwa.

Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba John Kabudi, alinukuliwa akiwatuhumu wakosoaji wa sheria hii, kuwa “mawakala wa mabeberu.”

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya katibu wa Bunge, katika mabadiliko hayo – Miscellaneous Amendments No.2 ya mwaka 2019 – mbali na sheria ya madini, serikali imepanga kufanyia mabadiliko Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya utozaji wa kodi za majengo.”

Katika mapendekezo hayo, serikali inasema, “…marekebisho ya Sheria ya Serikali za Mitaa ya utozaji wa kodi ya majengo, Sura ya 289. Lengo la marekebisho hayo, ni kuweka viwango mfuto vya kodi ya majengo nchini na kuiwezesha TRA kuwa mkusanyaji pekee wa kodi hiyo.

“Viwango vinavyopendekezwa ni Sh. 10,000 kwa majengo ya kawaida kwa maeneo ya mijini na vijijini; Sh. 20,000 kwa nyumba za ghorofa katika maeneo ya mijini.”

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema, serikali itarajie kupata upinzani mkali kutoka kwa wabunge katika kodi hiyo ya majengo, hasa kutokana na kuwa muswada umeletwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Uamuzi juu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi 13 Juni

Spread the love  MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), imepanga...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jeshi la Polisi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti

Spread the love  JESHI la Polisi Nchini limesema kuwa katika kukabiliana na...

KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Spread the love  MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya...

Habari za Siasa

Musoma Vijijini waomba ujenzi wa barabara uanze haraka

Spread the loveJIMBO la Musoma Vijijini, mkoani Mara, limeomba Serikali kuhakikisha ujenzi...

error: Content is protected !!