June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sheria kandamizi chanzo cha ukatili

Spread the love

SHERIA kandamizi za mirathi chanzo cha ukatili na unyanyasaji kwa wajane nchini, anaandika Regina Mkonde.

Kauli hiyo imetolewa leo na Rose Sarwat, Mkurugenzi wa Umoja wa Wajane Tanzania (TAWIA) katika Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

“’Timiza wajibu wako, mpe haki mjane’ hii ndio kauli mbiu inayoakisi umuhimu wa kufanya marekebisho ya sheria kandamizi hasa sheria za mirathi ambapo mjane haonekani kuwa na stahili katika mali za marehemu mumewe hata zile alizochangia kuzichuma,” amesema.

Ametolea mfano wa wanandoa wanaotalakiana kwamba mali walizochuma hugawanywa kadri ya mchango wa kila mmoja na kwamba ni tofauti kwa baadhi ya wajane kupata haki wakati waume zao wanapofariki kwa sababu mali zinatafsiriwa kuwa ni za marehemu pekee.

“Kuandika wosia ni jambo la muhimu litakalopunguza matatizo mengi ya wajane. Hata hivyo elimu ya kuandika wosia ni muhimu kwani wengine kwa kutojua wameandika wosia ambao hukataliwa hasa pale wanapowanyima warithi halali urithi au kutoa urithi wa mali isiyokuwa yao,” amesema.

Kwa upande wa Sihaba Nkinga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, amekiri kuwa kuna baadhi ya sheria zinazokwamisha upatikanaji wa haki za akina mama hususan wajane na kwamba serikali iko katika mkakati wa kuzifanyia marekebisho.

“Tanznaia katika kushughulikia masuala ya mirathi tunatumia sheria ya usimamizi wa mirathi ya mwaka 2011 na sheria za kimila za mwaka 1963 na kwamba pamoja na uwepo wa sheria hizo bado wajane wanakabiliwa na changamoto ya kupoteza haki katika usimamizi wa mirathi,” amesema Nkinga.

Ameongeza kuwa “aidha wakati mwingine wajane wamekuwa wakidhurumiwa mali na ndugu wa mume kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutojua haki zao, kuogopa kutengwa na ndugu wa mume, kuogopa gharama za kesi na wakati mwingine kutokuelewa taasisi zinazosaidia wanawake kisheria.”

Nkinga amewahakikishia wajane kwamba serikali inatambua upungufu wa sheria hizo na ina nia kubwa ya kuzifanyia marekebisho sheria mabazo bado zinakandamiza wanawake kwa maana ya kutoa haki stahiki na kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa sheria hizo zinaendana na halihalisi ya wakati wa sasa.

“Wanawake katika nchi nyingi duniani pamoja na Tanzania wanakumbwa na matatizo mengi yanayosababisha waishi kwa machungu na baadhi wakihangaika huku na kule kutafuta misaada ya kujikimu wanapofiwa na waume zao,” amesema.

Kufuatia changamoto hizo, Nkinga ameeleza kuwa wapo wanaojikuta katika mikono ya mila na desturi ambazo ni potofu kwa kutakiwa kurithiwa na ndugu wa waume zao na wakati mwingine hufanyiwa mila ya utakaso ambayo ni udhalilishaji mkubwa kwa mjane.

error: Content is protected !!