January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheria hii isaidie kudhibiti dawa za kulevya

Baadhi ya dawa za kulevya

Spread the love

HIVI karibuni Bunge lilitunga na kupitisha Sheria mpya ya Kupambana na Kuthibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015 (The Drugs Control and Enforcement Act, 2015). Anaandika Pendo Omary…(endelea).

Awali tatizo la dawa za kulevya lilianza kushamiri nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980. Katika miaka ya 1990, Serikali ilianzisha vitengo vya kudhibiti dawa za kulevya katika badhii ya idara na taasisi zake.

Taasisi hizo ni Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na idara ya Ushuru wa Fordha.

Licha ya kuwepo kwa vyombo hivyo tatizo liliendelea kukuwa, ndipo mwaka 1995, Bunge lilitunga Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.

Aidha, sheria hiyo bado haikukidhi matakwa, ndipo mwaka huu, Sheria mpya ikapitishwa na Bunge.

Utungwaji wa sheria hii, bilashaka utaleta mafanikio makubwa katika kudhibiti biashara ya dawa za kulevya ambayo imekuwa sugu nchini.

Mosi, Sheria iliyopo ina udhaifu wa adhabu, haitoi adhabu kulingana na ukubwa wa kosa kwenye baadhi ya makosa, hivyo kusababisha kukosekana kwa mizania ya haki. Sheria mpya imweka kima cha kuanzia cha adhabu iwe ni faini au kifungo, Kwa mfano;

Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha sheria iliyopo, adhabu ya kujihusisha na kilimo cha mimea ya dAwa za kulevya (mfano bangi) ni faini ya Sh. 1,000,000 au kifungo kisichozidi miaka 20.

Sheria mpya imeweka adhabu ya faini isiyopungua milioni 50 na isiyozidi milioni 500 au kifungo kisichopungua miaka 7 na kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja.

Adhabu ya kosa la kufadhili biashara haramu ya dawa za kulevya katika sheria ya sasa ni faini ya Sh. 10 milioni. Sheria mpya imeweka adhabu ya Sh. bilioni moja au kifungo kisichopungua miaka 30 au vyote kwa pamoja mbali na kutaifishwa kwa mali za mfadhili.

Kwa upande wa makosa ya kusafirisha na kufanya biashara ya dawa za kulevya, sheria ya sasa imetoa adhabu ya faini au kifungo cha maisha. Sheria mpya imeweka adhabu ya kifungo cha maisha peke yake. Lengo ni kuondoa uwezekano wa wahalifu kupewa adhabu ya faini ambayo ni rahisi kuilipa.

Pili, sheria mpya imeharamisha umiliki wa mitambo au maabara inayotumika kutengeneza dawa za kulevya. Adhabu kali kwa kosa hili ni kifungo cha maisha na faini isiyopungua Sh. 200 milioni.

Tatu, Sheria mpya imetoa mamlaka ya kushughulikia uhalifu wa dawa za kulevya nje ya mipaka ya Tanzania katika vyombo vya usafiri wa majini na angani na bahari kuu.

Nne, Sheria mpya imetoa adhabu ya faini au kifungo jela ili kuwadhibiti watendaji waliopo katika udhibiti wa dawa za kulevya wanaokiuka maadili ya kazi, jambo ambalo haliko katika sheria iliyopita.

Tano, Sheria mpya imeweka fomu maalum ambazo hazipo kwenye sheria inayotumika sasa. Fomu hizi zitaondoa ulazima wa kumtafuta shahidi ambaye wakati mwingine hawezi kupatikana kiurahisi, hivyo kuongeza kasi katika kuendesha mashtaka.

Sita, Sheria mpya imeweka adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 kwa watuhumiwa watakaowashawishi au kuwahusisha watoto kujiingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya tofauti na sheria ya sasa ambayo ipo kimya.

Saba, Sheria mpya imeanzisha mfuko wa kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya. Baadhi ya vyanzo vya mapato vya mfuko huo vitatokana na fedha itakayoidhinishwa na Bunge, mapato ya mali zinazotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya zilizofilisishwa, misaada, mikopo na michango ya hiari.

Mbali na hayo Sheria mpya imeainisha vyema masharti kwamba serikali itakuwa na wajibu wa kuchukua hatua kuhusu udhibiti wa dawa za kulevya. Ikiwemo uanzishwaji wa vituo vya tiba kwa watumiaji na waathirika wa dawa za kulevya.

 

error: Content is protected !!